Ticker

6/recent/ticker-posts

Bernard Morrison Asema baada ya kuwakosa Zalan FC sasa yupo fiti kuwakabili Al Hilal ya Sudan

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

WINGA wa Yanga Bernard Morrison baada ya kukosekana katika michezo miwili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini, amesema yupo fiti kurejea uwanjani kuwakabili Al Hilal ya Sudan.

Morrison hakuonekana katika michezo hiyo miwili kutokana na kusumbuliwa na majeraha, lakini Yanga ilifanikiwa kutinga raundi ya kwanza kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0, ikishinda 4-0 mechi ya kwanza na 5-0 katika mechi ya pili ya marudiano.

Morrison ambae amepona na kurejea uwanjani hivi karibuni, Amesema kwa kushirikiana na wachezaji wenzake atahakikisha anapambana kuisaidia timu yao kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa hadi kufikia malengo ya msimu huu.

Alisema malengo yao makubwa ni kuona Yanga inacheza hatua ya robo fainali ya michuano hiyo na anaimani hilo litafanikiwa kwa sababu ya ubora wa kikosi cha timu yao.

"Ni kweli sijaonekana uwanjani kwa sababu ya majeruhi na sasa niko vizuri, nimeanza mazoezi na nitarudi uwanjani kupambania timu kupata matokeo mazuri katika michezo iliyopo mbele yetu," alisema Morrison.

Wakati Morrison akishuka na 'mistari' hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa atatumia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting kurekebisha madhaifu yao kuelekea mchezo huo dhidi ya Al Hilal watakaoanzia nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 8, mwaka huu.

Kabla ya kucheza mchezo huo Oktoba 3, Yanga itacheza mchezo wa tano wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Nabi amesema kikosi chake kimeanza mazoezi  kujiandaa na michezo mitatu iliyo mbele yao huku akiitumia mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting kujiimarisha na kufanyia kazi mapungufu yao kabla ya kukutana na Al Hilal.

Alisema Ruvu Shooting si timu mbaya, lakini kwa kuwa wanakwenda katika mashindano makubwa wanapaswa kuwa na mchezo kabla ambao utampa majibu ya nini anatakiwa kufanya.

"Katika michezo yote hii tunahitaji ushindi, mchezo dhidi ya Ruvu Shooting tutatakiwa kupambana kupata mabao mengi ili niweze kuona mapungufu yaliyopo hasa ukiangalia tutakuwa tumetoka kwenye mapumziko kutokana na michezo ya timu za taifa," alisema Nabi.

Alisema mazoezi wanayofanya yatakuwa wanayatumia kumaliza mapungufu yao ili kuandaa kikosi imara kwa ajili ya kutafuta matokeo mazuri katika mchezo wao dhidi ya Al Hilal ili kufikia malengo yao ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.

Nabi alisema wachezaji wake watakuwa wanafanya mazoezi na kurudi nyumbani hadi mwisho wa mwezi huu watakapoingia kambini kujiandaa na mechi hiyo ambayo itakuwa ya ushindani mkubwa kwa sababu ya Al Hilal kuwa na uzoefu wa muda mrefu katika michuano hiyo.

"Tumepata matokeo mazuri mechi iliyopita, ila kuna mapungufu tumeyaona ikiwamo safu ya ushambuliaji kwa kutengeneza nafasi na kushindwa kuzitumia, sasa tunarudi uwanjani kufanyia kazi hilo na mechi yetu dhidi ya Ruvu Shooting itatupa taswira ya mchezo wetu wa kimataifa," alisema Nabi.

Post a Comment

0 Comments