Ticker

6/recent/ticker-posts

‘Robertinho’ Awaondoa Hofu Mashabiki Wa Simba Asema Ushindi Lazima

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kusema kikosi chake kitaingia na mbinu tofauti kuwakabili wapinzani wao, Raja Casablanca kwa sababu wanahitaji ushindi.


Robertinho alisema aina ya uchezaji ya ugenini na nyumbani huwa na tofauti kubwa, hivyo wamejiandaa kushambulia zaidi.


Kocha huyo anataka kuona vijana wake wakicheza kwa kasi kubwa dakika zote 90 ili kuhakikisha wanazibakisha pointi tatu nyumbani.


Alieleza walipocheza dhidi ya Horoya AC aliwataka wachezaji kujilinda na  kushambulia kidogo na baada ya kufungwa bao pekee katika mchezo huo walifunguka kwa kuwashambulia wenyeji ili kusaka goli la kusawazisha.


“Nimepanga kuifanyia maboresho safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Moses Phiri, John Bocco, Jean Baleke, Pape Sakho, Clatous Chama na Kibu Denis ili kuhakikisha tunapata ushindi wa mabao mengi nyumbani. Nataka kuona wachezaji wangu wakilishambulia goli la mpinzani wetu mara nyingi zaidi kwa maana ya kuanzia dakika ya kwanza hadi 90, kila mchezo wa nyumbani,” alisema Robertinho. 


Alisema hatua waliyofika katika mashindano hayo kila timu inatakiwa kupambana kupata ushindi nyumbani na kutafuta sare ugenini.


"Tunahitaji matokeo ya ushindi katika mchezo dhidi ya Raja Casablanca, kupata matokeo hayo tutalazimika kuingia na mbinu tofauti na tulivyoingia kwenye mechi iliyopita," Robertinho alisema.


Kuelekea mechi dhidi ya Raja Casablanca,Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally alisema wataingia kwa tahadhari katika mechi hiyo, ingawa haamini kama wapinzani wao watabadilisha mfumo ambao wamezoea kuucheza.


"Tahadhari ni muhimu, mchezo ni mgumu, ila sisi tunakwenda kutafuta matokeo mazuri, tunajua mpira wa barani Afrika umebadilika, lakini timu za Afrika Kaskazini ambazo tunaziita za Kiarabu hadi leo bado hazijabadilisha mfumo wao wa uchezaji, bado kwa kiasi kikubwa sana wanategemea kushinda kwenye viwanja vyao vya nyumbani, Al Ahly, pamoja na ubora wake wote, huwezi kuona ubora wake wa asilimia 100 wakiwa viwanja vya ugenini, labda kama ametanguliwa kufungwa ndiyo unamwona anaanza kufurukuta na kututumka.


Akirudisha bao anarudi tena kwenye aina yake ya uchezaji wa taratibu na kupoteza muda, mechi yake anayotegemea ni ile ya nyumbani. Hivyo hivyo kwa Raja Casablanca, hatutegemei kama anaweza kuja hapa akacheza kwa kasi kubwa kama anavyocheza kwao, lakini vyovyote itakavyokuwa sisi Simba tumejidhatiti iwavyo ilivyo, tuhangaike naye kuanzia dakika ya kwanza hadi 90 kwa kasi ya hali ya juu, tumepelekee moto kweli kweli, mwisho wa siku tupate pointi tatu," alisema Ahmed.


Simba ambayo ipo katika Kundi C,  inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Horoya ya Guinea, wakati vinara wa kundi hilo wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kuitwanga Vipers SC ya Uganda mabao 5-0.


Post a Comment

0 Comments