HATIMAYE mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na kiungo, Feisal Salum 'Fei Toto' wamemalizana baada ya kiungo huyo kusaini mkataba mpya wa Sh. milioni 350 ili kurejea Jangwani.
Taarifa za uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema viongozi wa Yanga walikwenda Zanzibar kufanya mazungumzo na mchezaji huyo na kufikia makubaliano mapya.
Habari za kina ni kwamba baada ya mazungumzo hayo, wamekubaliana kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya Sh. milioni 350 na atalipwa mshahara wa Sh. milioni 15 kwa mwezi.
Baada ya kukamilisha makubaliano hayo mapya, sasa Fei Toto anatarajia kuingia kambini baada ya Yanga kumaliza mchezo wake wa mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), utakaochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Imeelezwa Yanga imefikia uamuzi huo ili kuongeza nguvu katika kikosi chake kwa ajili ya kuhakikisha wanafikia malengo ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA pamoja na kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema nyota huyo anatakiwa kurejea katika majukumu ya klabu kwa ajili ya kulinda kipaji chake na manufaa kwa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).
Nabi alisema Fei Toto ni mchezaji wa kutegemewa wa Yanga na Taifa Stars na kumalizika kwa sakata lake ni jambo la faraja.
Fei Toto alitangaza kuvunja mkataba wake na Yanga kwa kuilipa kiasi cha Sh. milioni 112 lakini shauri hilo lilipopelekwa katika Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliamuru nyota huyo bado ni mchezaji wa klabu hiyo ya mitaa ya Jangwani na Twiga.
Fei Toto amekuwa nje ya kikosi cha Yanga tangu Novemba mwaka jana na presha ya madai yake ya kuboresha mshahara wake ilishika kasi zaidi wakati dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa.
Katika muda ambao hakuwa na kikosi cha Yanga, Fei Toto, alionekana amekwenda Dubai kwa ajili ya mapumziko ya muda mfupi kabla ya kurejea nchini kusikiliza shauri lililokuwa linamkabili.
Mapema mwaka huu nyota huyo alionekana akifanya mazoezi na timu yake ya zamani ya JKU ambayo ilikuwa ikijiandaa na mashindano ya Kombe la Mapinduzi huko Visiwani Zanzibar.
0 Comments