Ticker

6/recent/ticker-posts

NYOTA WA WIKI: Lionel Messi

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KUNA wachezaji 832 kutoka mataifa 32 nchini Qatar wakati huu wa kushiriki Kombe la Dunia litakalofanyika Novemba 20 hadi Desemba 18.

Supastaa Lionel Messi ametiwa katika orodha ya wachezaji ambao kampuni za kamari zimebashiri ataibuka mfungaji bora.

Nchi yake ya Argentina pia imetiwa katika kundi la mataifa matano yanayopigiwa upatu kutwaa taji ambalo lina Brazil, Ufaransa, Uingereza na Uhispania.

Mshambulizi huyo wa Paris Saint-Germain mwenyewe ameacha nje Argentina katika orodha yake ya timu anaamini zitabeba kombe. Orodha yake ina Brazil, Uingereza na Ufaransa.

Katika makala haya ya 22, Messi atakuwa akitafuta taji hilo moja ambalo hana katika kabati lake. Amefagia La Liga, Copa del Rey, Klabu Bingwa Ulaya na Klabu Bingwa Duniani akiwa FC Barcelona, Ligue 1 akichezea PSG na Olimpiki, Copa America na CONMEBOL-UEFA Cup of Champions (Finalissima) akivalia jezi ya Argentina.

Messi ana tuzo nyingi za kibinafsi zikiwemo tisa za mwanasoka bora duniani, kiatu cha dhahabu barani Ulaya (sita) na ni mwanasoka bora nchini Argentina (14), miongoni mwa nyinginezo nyingi.

Wachanganuzi wanaamini atazima mjadala wa nani ni mwanasoka bora katika historia ya mchezo huu akifaulu kutawala Kombe la Dunia 2022 linaloweza kuwa lake la mwisho kabla astaafu.

Messi atakuwa na miaka 39 wakati wa Kombe la Dunia 2026 kwa hivyo makala haya ni fursa ya mwisho kutafuta taji ambalo limemponyoka.

Yeye ndiye mfungaji bora wa Argentina akiwa na mabao 91 na pia amechezea taifa hilo mechi nyingi kuliko wote (165).

Messi anafahamika kwa kasi yake ya kutisha, kulisha wapinzani chenga, kusuka pasi za uhakika na pia kumwaga makipa, hasa akitumia mguu wake hatari wa kushoto.

Ni mchezaji tunayeamini ana uwezo wa kufikisha Argentina mbali katika mashindano haya makubwa duniani. Makali yake yataanza kupimwa katika mechi za makundi dhidi ya Saudi Arabia, Mexico na Poland.

Post a Comment

0 Comments