Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Brazil waifunga Uswisi Na Kuingia Hatua Ya 16-Bora

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

CASEMIRO alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 ulioupata Brazil dhidi ya Uswisi katika mechi ya Kundi G uwanda wa makontena 974 mnamo Jumatatu na kusaidia miamba hao kutinga hatua ya 16-bora.

Kiungo huyo wa Manchester United, alipachika wavuni bao hilo kunako dakika ya 83 baada ya kumzidi ujanja kipa Yann Sommer.

Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Brazil kusajili baada ya kufungua kampeni zao za Kundi G kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Serbia mnamo Novemba 24, 2022. Mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia sasa watafunga michuano ya makundi dhidi ya Cameroon mnamo Disemba 2 uwanjani Lusail Iconic.

Bao ambalo nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr, alifungia Brazil katika dakika ya 60 halikuhesabiwa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba lilijazwa kimiani akiwa ameotea.

Chini ya kocha Murat Yakin, Uswisi sasa watakamilisha mechi zao za Kundi G kwa kumenyana na Serbia ugani 974 mnamo Disemba 2, 2022.

Brazil wanaopigiwa upatu wa kunyanyua Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka huu, sasa wameshinda mechi zote 17 zilizopita za hatua ya makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Mechi dhidi ya Uswisi ilikuwa ya tisa mfululizo kwa Brazil kushinda katika mapambano yote. Miamba hao ambao wamefunga mabao 29 kutokana na mechi hizo, hawajapoteza mchuano wowote tangu Argentina iwapige 1-0 kwenye fainali ya Copa America 2021.

Pigo kubwa kwa Brazil wanaojiandaa kuvaana na Cameroon, ni kutokuwepo kwa supastaa wa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr atakayekosa pia mechi hiyo ya mwisho ya Kundi G. Neymar, 30, aliondolewa uwanjani katika dakika ya 80 Alhamisi iliyopita baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu akiwajibika dhidi ya Serbia.

Post a Comment

0 Comments