Ticker

6/recent/ticker-posts

Phiri aendelea kung'ara kwa Mkapa

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Mshambuliaji wa Simba Mzambia, Moses Phiri amezidi kung'ara kunako  Ligi Kuu ya NBC baada ya kufanikiwa kuifungia timu yake ya Simba bao la kuongoza katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC.

DAKIKA 45 za kipindi cha kwanza za mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa tatu zilitamatika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji Simba kuongoza bao 1-0 dhidi ya KMC.

Bao la Simba liliwekwa kimiani na mshambuliaji, Moses Phiri dakika ya tatu tu ya mchezo baada ya kuwazidizi ujanja mabeki wa KMC wanaoongozwa na Andrew Vicent 'Dante' na Ibrahim Ame.

Hili ni bao la tatu kwa Phiri msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara tangu aanze kukitumikia kikosi hicho akimfikia mshambuliaji wa Namungo, Reliants Lusajo mwenye mabao matatu pia.

Mchezo huu ulianza kwa kasi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu huku wenyeji Simba wakionekana kutengeneza mshambuzi mengi na yenye hatari zaidi ya wapinzani wao KMC.

Eneo la kiungo kwa pande zote mbili ndilo ambalo limeonekana kuchangamsha mchezo kwani KMC chini ya Kocha wake Mkuu, Thierry Hitimana imeanza na viungo, Baraka Majogoro, Styve Nzigamasabo na Emmanuel Mvuyekure.

Kwa upande wa Simba chini ya kaimu Kocha Mkuu, Selemani Matola imeanza na Sadio Kanoute na Nassoro Kapama huku wakisaidiwa na viungo washambuliaji, Clatous Chama na Augustine Okrah.

Uwepo wa Matteo Antony kwenye benchi la KMC huenda ukaongeza makali kwenye ushambuliaji wa timu hiyo kipindi cha pili kwani licha ya kumtegemea, Darueshi Saliboko ila bado ameshindwa kupenya ngome ya Simba inayoongozwa na Henock Inonga na Mohamed Ouattara.

KMC imeingia kwenye mchezo huu ikiwa na rekodi mbovu dhidi ya Simba kwani tangu imeanza kucheza rasmi Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/2019 haijawahi kushinda wala kutoa sare.

Katika michezo nane iliyopita ya Ligi Kuu Bara waliyokutana Simba imeshinda yote huku ushindi mkubwa ukiwa ni ule wa mabao 4-1, mechi iliyopigwa katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora Desemba 24 mwaka jana.

Post a Comment

0 Comments