Ticker

6/recent/ticker-posts

Jezi Mpya za simba zavunja rekodi haijawahi kutokea

 Jezi Mpya za simba zavunja rekodi haijawahi kutokea

"JEZI za msimu mpya za Klabu ya Simba zimeweka rekodi kwa mashabiki wa soka kugombea kununua hadi Jeshi la Polisi kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya katika duka la mdhamini wa jezi hizo, Fred Vunjabei lililoko Sinza Madukani, Dar es Salaam."

Mashabiki wa Simba jana walitia fora baada ya kumiminika kwa wingi katika duka la Vunjabei wakitaka kununua jezi mpya kwa ajili ya Tamasha lao la Simba Day leo.

Mzigo huo ulianza kuuzwa rasmi jana baada ya kuchelewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kubadili mdhamini kutoka SportPesa na kuingia mwingine ambaye ni M-BET zoezi ambalo lilifanya kuchelewa kuwasili.

Kutokana na umati huo na kila mmoja kuhitaji kuingia ndani kupata nafasi ya kununua jezi hizo mpya, ilisababisha tafrani na vurugu kwa mashabiki hao, hivyo kusababisha watu wa usalama kupiga bomu la machozi ili kuleta utulivu.

Pamoja na jezi hizo kuchelewa kuingia sokoni, lakini mashabiki wa timu hiyo walionekana kuvutiwa zaidi kila mmoja akitamani kubeba aina zote tatu licha ya kutakiwakununua moja moja ili kila mmoja aweze kupata.

Mmoja wa mashabiki waliojitokeza dukani hapo, Rashid Mtambo, alisema misimu yote Simba wanakuwa na jezi kali ila ya msimu huu ni balaa zaidi.

“Simba huwa hatuna jambo dogo, miaka yote tumekuwa na jezi kali ila ya msimu huu ni zaidi ya balaa na unaweza kutinga na kwenda nayo kwa wakwe zako,” alisema Rashid.

Katika hatua nyingine Simba imemtambulisha mshambuliaji mpya raia wa Serbia, Dejan Georgijević aliyekuwa akiichezea NK Domžale ya Slovenia.

Dejan mwenye umri wa miaka 28, ambaye amefunga mabao manne katika mechi 17 za msimu uliopita, amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Simba na atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaotambulishwa leo katika Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.  

Kwingineko mshambuliaji wa Vipers ya Uganda, Cesar Manzoki, ambaye alitarajiwa kutua Simba, aweka wazi kuwa amebakiza mkataba wa miezi miwili unaofikia tamati Oktoba mwaka huu na sio 2025 kama waajiri wake hao wanavyodai.

Manzoki anatajwa kumalizana na klabu ya Simba huku uongozi wa Vipers kupitia Ofisa Habari wao, Wasike Abdu, akidai kwamba nyota huyo bado ni mchezaji wao halali kwa kuwa wana mkataba naye hadi 2025.

Akizungumza jana katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, kabla ya timu ya Vipers kuelekea nchini kwao Uganda, Monzoki, alisema hakuna ukweli juu ya mkataba wake na kwamba ulikuwa wa miaka miwili ndani ya klabu yake ya sasa ambao unamalizika Oktoba.

Alisema Meneja wake na viongozi wa Simba wako mezani wanazungumza kwa ajili ya kusaini mkataba kuitumikia klabu hiyo na tayari wamepeleka barua Vipers kwa ajili ya kununua mkataba wake kwa muda uliobakia.

“Huo sio ukweli kwamba mkataba wangu ni miaka miwili ndani ya Vipers, nimebakiza miezi miwili na Oktoba namaliza na klabu yangu, lakini kuhusu Simba, meneja wangu na Simba wako katika mazungumzo mazuri.

“Malengo yangu ni kucheza Simba, kama mambo yakienda vizuri basi nitakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo, kuhusu kutocheza mechi dhidi ya Yanga ni kwa sababu ya kutojisikia vizuri,” alisema Manzoki ambaye alikuwa hapa nchi na timu yake ya Vipers kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Yanga katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi na wageni hao kushinda mabao 2-0.


Post a Comment

0 Comments