Ticker

6/recent/ticker-posts

Man Utd chini ya Erik ten Hag waanza Msimu Mpya kwa Kichapo kutoka kwa Brighton


BRIGHTON walimkaribisha kocha Erik ten Hag wa Manchester United kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hapo jana kwa kichapo cha 2-1 katika uwanja wa Old Trafford.

Wachezaji wapya wa Man-United – Christian Eriksen na Lisandro Martinez walipangwa katika kikosi cha kwanza huku Cristiano Ronaldo aliyeibuka mfungaji bora wa mabingwa hao mara 20 wa EPL muhula jana kwa mabao 18 akiingia katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Fred.

Pascal Gross alipachika wavuni mabao yote mawili ya Brighton katika kipindi cha kwanza kabla ya vijana wa Ten Hag kufutwa machozi na Alexis Mac Allister aliyejifunga katika dakika ya 68.

Ushindi wa Brighton uliendeleza ubabe wao dhidi ya Man-United waliopokea kichapo cha 4-0 kutoka kwa kikosi hicho cha mkufunzi Graham Potter mnamo Mei katika uwanja wa Amex.

Ulikuwa pia ushindi wa kihistoria kwa Brighton walioshuka dimbani wakiwa wamepoteza mara nane na kuambulia sare moja kutokana na mechi tisa za awali dhidi ya Man-United ugenini.

Matokeo ya jana ya Man-United yalirejesha kumbukumbu za 2014 ambapo kocha wao wa zamani, Louis van Gaal, alikaribishwa pia EPL kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Swansea City uwanja wa Old Trafford.

Post a Comment

0 Comments