Ticker

6/recent/ticker-posts

Yanga Yaanza Kujipanga Mashindano Ya Kimataifa

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Yanga Yaanza Kujipanga Na Mashindano Ya CAF

 


BAADA ya kumaliza msimu wa 2021/2022 kibabe, uongozi wa Yanga umesema mchakato wa uchaguzi unaoendelea ndani ya klabu yao hautaathiri kwa namna yoyote maandalizi ya timu kuelekea katika msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki.

Yanga imemaliza msimu kwa kuchukua Ngao ya Jamii, taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Kombe la FA, ambayo yote yalikuwa yanashikiliwa na watani zao, Simba.

Akizungumza jijini jana, Ofisa Mtendaji  Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha, alisema licha ya klabu kuwa katika mchakato wa uchaguzi, sekretarieti ya klabu hiyo imejiandaa kukamilisha shughuli mbalimbali za kiutawala ili kutoharibu programu zilizoandaliwa.

Senzo alisema kamwe mchakato huo wa uchaguzi hauna nguvu ya kuathiri mikakati yao kwa sababu wanahitaji kuona Yanga inafanya maandalizi sahihi kwa ajili ya kupeperusha vyema bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa na ligi watakayoshiriki.

Alisema timu yao inatarajia kwenda Uturuki kwa ajili ya kufanya maandalizi ya msimu ujao na wanaamini kambi hiyo itawaimarisha na kuwajenga nyota wake ili kukabiliana na ushindani watakaokutana nao.

Aliongeza kuhusu usajili tayari Yanga inaelekea kwenye hatua ya mwisho na inawataka wanachama na mashabiki wake kuwa watulivu kwa sababu imezingatia mapendekezo ya benchi la ufundi.

"Suala la usajili halina mashaka kwa sababu tayari tumeshakamilisha kwa asilimia 80, na kazi iliyopo kwetu ni kuangalia ni sehemu gani ambayo timu itaenda kuweka kambi kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao.

“Kila kitu kipo vizuri, kilichobakia ni muda wa kutambulisha wachezaji na kwa asilimia kubwa tumefanya usajili kulingana na mahitaji ya kocha Nabi (Nesredine ), hasa kuangalia zaidi kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa ,” alisema Senzo.

Aliongeza kwa sasa wanahitaji kujipanga kuendelea pale walipoishia na ni kupeperusha vizuri bendera ya klabu yao  katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

“Msimu ujao tunahitaji kulinda haya makombe yetu kwa kujipanga vizuri, lakini msimu huu haukuwa mzuri katika michuano ya kimataifa, tumejifunza kitu na tunaenda kufanyia kazi pale tulipokosea na msimu ujao tutafika mbali katika michuano ya Afrika,” alisema Senzo.

Ofisa huyo alisema changamoto waliyokuwa nayo msimu uliopita kwa kushindwa kutumia baadhi ya wachezaji wao wa kigeni kwa sababu hati zao za uhamisho za kimataifa (ITC) zilichezewa,  kitu hicho hakitajirudia.

Yanga itaanza michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua za awali huku ikifurahia kupatikana kwa wachezaji wake wa kimataifa ambao ni Yannick Bangala, Fiston Mayele na Khalid Aucho, waliokosekana msimu huu ambao walitolewa mapema.

Mbali na Yanga, timu nyingine kutoka Tanzania Bara zitakazoshiriki mashindano ya kimataifa ni Simba itakayochuana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam FC na Geita Gold FC kutoka mkoani Geita zenyewe zitaenda kuchuana katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wakati huo huo, mgombea wa nafasi ya urais, Hersi Said amesema mshambuliaji wao, Fiston Mayele hatauzwa na kuwataka mashabiki wa Yanga kutokuwa na hofu.

Hersi alisema pia suala la nidhamu ya wachezaji litaimarishwa na litaendelea kusimamiwa na menejimenti ya klabu na kuahidi mambo mazuri yataendelea kuwamo ndani ya klabu yao katika msimu ujao.

Yanga itafungua msimu mpya kwa kucheza na Simba katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayochezwa Agosti 13, mwaka huu wakati Agosti 17, mwaka huu kipenga cha msimu wa 2022/2023 kitaanza rasmi.


Post a Comment

0 Comments