Ticker

6/recent/ticker-posts

Simba: Tunasajili kisasa

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

UONGOZI wa Klabu ya Simba umesema unaendesha mchakato wa usajili wa wachezaji wapya 'kisasa' na kamwe hautashinikizwa na presha yoyote ya ushindani kama ilivyozoeleka.


Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema klabu yake itasajili wachezaji wapya kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa kufuata mahitaji halisi yaliyopendekezwa na benchi la ufundi si vinginevyo.

Ahmed alisema tayari mchakato huo umeshakamilika kwa asilimia kubwa na muda wa kuwatangaza ukifika watawaweka hadharani.

Alisema wanaamini Simba itakuwa na kikosi imara kwa sababu usajili wao umefanyika kwa umakini ili kufikia malengo ambayo yamechagizwa na uzoefu walioupata kwenye michuano ya kimataifa.

"Kwa wenzetu utambulisho wa wachezaji ni biashara, siku ya utambulisho hurejesha sehemu ya gharama za usajili na mauzo ya jezi, sisi bado hatujafikia huko lakini ni lazima tuanze kidogo kidogo kufanya biashara na wachezaji," Ahmed alisema.

Aliongeza pia klabu yake imeandaa utaratibu mzuri wa kutambulisha wachezaji katika muda rafiki kwa sababu inawathamini mashabiki na wanachama  wake.

Simba ilimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2021/2022 katika nafasi ya pili wakati kwenye mashindano ya Kombe la FA ilitolewa hatua ya nusu fainali kwa kufungwa na watani zao Yanga huku kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika iliishia robo fainali.


Post a Comment

0 Comments