Ticker

6/recent/ticker-posts

Sadio Mane Ashinda Tuzo Ya Mchezaji Bora Barani Afrika 2022

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

  • Straika wa Bayern Munich Sadio Mane ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika
  • Mane alifunga penalti za ushindi Senegal ikishinda AFCON na vilevile kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia 
  • Mane aliwapiku Edouard Mendy (kipa wa Chelsea na Senegal) na Mohamed Salah (mshambuliaji wa Liverpool na Misri)


Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Senegal Sadio Mane ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika.

Mane alikabidhiwa tuzo hiyo katika hafla iliyoandaliwa jijini Rabat nchini Morocco na kuishinda tuzo hiyo kwa mwaka wa pili mfululizo baada ya kuitwaa mwaka jana. 

Mane alifunga penalti ya ushindi na kuisaidia Senegal kushinda kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza kwa kuwanyuka miamba wa AFCON Misri kupitia mikwaju ya penalti.

“Nimefurahi sana kupokea tuzo hii mwaka huu,” Mane alisema akipokea tuzo hiyo. 

Mshambuliaji huyo aliwapiku Edouard Mendy (kipa wa Chelsea na Senegal) na Mohamed Salah (mshambuliaji wa Liverpool na Misri) kutwaa tuzo hiyo. 

Mane ambaye ameiaga klabu ya Liverpool na kujiunga na miamba wa Ujerumani Bayern Munich kwa mkataba wa miaka mitatu, pia aliisaidia Senegal kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia nchini Qatar baadaye mwaka huu. 

Ilivyokuwa katika fainali ya AFCON, Mane alifunga penalti ya ushindi na Senegal kuwatandika Misri ili kufuzu kwa mashindano hayo ya ulimwengu. 

“Ninataka kuwashuruku watu wa Senegal na ninatoa tuzo hii kwa vijana wa taifa langu,” alisema Mane, ambaye alishinda vikombe viwili na Liverpool msimu jana. 

Tuzo ya mane ni moja tu kati ya tuzo tano zilizoshindwa na Senegal katika jumla ya vitengo saba vya tuzo za wanaume. 

Kocha wa Senegal Aliou Cisse alishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka, timu yake kutajwa timu ya mwaka ya wanaume, Pape Sarr kutajwa mchezaji mchanga bora zaidi huku Pape Ousmane Sakho (raia mwengine wa Senegal) akishinda tuzo ya bao bora zaidi alilofungia klabu yake ya Simba katika Champions League ya Afrika. 

Mane sasa anaingia katika orodha ya wanasoka sita ambao wameibuka wanasoka bora mara mbili. Wengine ni Salah 2017 & 2018), Didier Drogba (2006 & 2009), Roger Milla (1976 & 1990), Nwankwo Kanu na El Hadji Diouf (2001 & 2002).

George Weah na Abedi Pele walinyakua tuzo hiyo mara tatu nao Samuel Eto’o na Yaya Toure mara nne.

Washindi wa tuzo za CAF 2022: Mwanasoka bora wa mwaka (mwanamume): Sadio Mane (Senegal & Bayern Munich); Mwanasoka bora wa mwaka (mwanamke) Asisat Oshoala (Nigeria & Barcelona); Kocha bora (mwanamume) Aliou Cisse (Senegal); Kocha bora (mwanamke) Desiree Ellis (Afrika Kusini); Timu ya taifa ya mwaka (wanaume) Senegal; Timu ya taifa ya mwaka (wanawake) itachaguliwa baada ya fainali ya Kombe la Afrika (Wafcon) kati ya Afrika Kusini na wenyeji Morocco leo Jumamosi; Chipukizi bora wa mwaka (mwanamke) Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas/Alvaldsnes); Chipukizi bora wa mwaka (mwanamume) Pape Matar Sarr (Senegal & Tottenham Hotspur); Klabu bora ya mwaka (wanawake) Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini); Klabu bora ya mwaka (wanaume); Wydad AC (Morocco); Mchezaji bora wa klabu za Afrika (mwanamke) Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas/Alvaldsnes); Mchezaji bora wa klabu za Afrika (mwanamume) Mohamed El Shenawy (Misri & Al Ahly); Bao kali la mwaka Pape Ousmane Sakho (Senegal & Simba).

Post a Comment

0 Comments