Ticker

6/recent/ticker-posts

Okwa atua Misri Aongeza mzuka Simba

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KIUNGO mpya wa Simba, Mnigeria Nelson Okwa wikiendi iliyopita aliiaga timu aliyokuwa akiichezea ya Rivers United kibabe kwa kuiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, kisha mapema anaanza mchakato wa safari ya kwenda kuanza maisha mapya ndani ya kambi ya Simba iliyopo Ismailia, Misri.


Okwa ni mmoja ya nyota wapya waliosajiliwa na Simba kwenye dirisha hili la usajili litakalofungwa Agosti 31 na mara baada ya mechi ya mwisho na Rivers iliyoitoa Yanga kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, aliwaaga wenzake na benchi la ufundi na fasta jana alichukua usafiri wa ndege kutoka Mji wa Port Harcourt alipokuwa na timu yake ya Rivers kisha akatua Abuja kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusafiri kwenda kambi ya Misri.

Taarifa kutoka Nigeria, zinasema Okwa alibidi afike kwanza Abuja kutokana na kuhakikisha anapata visa ya kuingia Misri ilipo kambi ya timu yake mpya ya Simba ambayo kwa mujibu wa Kocha Zoran Maki itakuwa ya wiki tatu na itacheza mechi zisizopungua tano kabla ya kurejea nchini Agosti 5.

Inaelezwa muda wowote kuanzia sasa kama Okwa atapata visa atatumiwa tiketi ya ndege na mabosi wake wapya wa Simba kisha atatua Misri kwa ajili ya kutambulishwa kama mchezaji mpya wa timu hiyo.

Baada ya zoezi hilo la kutambulishwa kukamilika atajiunga moja kwa moja kwenye mazoezi na wachezaji wenzake kama ambavyo Mwanaspoti lilikujuza siku nyingi juu ya usajili wake na wengine wakafuata upepo.

Okwa alipotafutwa na Mwanaspoti, alikiri yupo Nigeria kwa ajili ya mambo yake mengine na kama atakuwa mchezaji mpya wa Simba msimu ujao basi hilo si jukumu lake kuweka wazi.

“Ishu ya kuwa mchezaji mpya wa Simba basi viongozi wangu ndio wana haki ya kuliweka hilo wazi lakini kwa sasa nipo kukamilisha mambo yangu binafsi hapa Abuja, hayo mengine tuyaache kwanza,” alisema Okwa anayefahamika nchini kutokana na kiwango bora alichoonyesha wakati alipocheza mechi mbili dhidi ya Yanga.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema kikosi chao bado hakijamaliza zoezi la usajili kwani kuna wachezaji wengine wapya kama si wawili basi watatu watawatangaza baada ya kukamilisha taratibu zao.

“Viongozi wanaendelea na zoezi la usajili, kama likikamilika ndani ya muda mfupi tutawatangaza wachezaji hao wawili au watatu wapya ambao watajiunga nasi huku Misri. Mashabiki waendelee kutuombea dua ili tufanye vizuri msimu ujao katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa,” alisema.

Post a Comment

0 Comments