Ticker

6/recent/ticker-posts

Coastal Union FC Yatua Arusha

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Coastal Union FC Yatua Arusha


Arusha. Wakati mabingwa wa ligi Kuu Bara msimu wa 2021/22 Yanga SC ikipanga kuwasili usiku wa leo Juni 30 jijini hapa kwa ajili ya mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho la Azam Sports (ASFC) wapinzani wao Coastal Union FC wao wanawasubiri baada ya kufika mapema.

Mchezo huo utapigwa Jumamosi Julai 2 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa ambapo inakuwa ni mchezo wa pili wa ASFC timu hizo kukutana mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 kwenye mchezo wa nusu fainali iliyopigwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1.

Coastal Union wametinga fainali baada ya kuifunga Azam FC goli 6-5 katika mikwaju ya penati kwenye mchezo wa nusu fainali huku Yanga wenyewe wakitinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga Simba SC bao 1-0.

Ofisa habari wa Coastal Union FC, Jonathan Tito amesema timu hiyo tayari iko hapa kwa ajili ya maandalizi ya mwisho mwisho kuwakabili Yanga katika mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa mgumu kutokana na ubora wa vikosi vyote.

"Hatuko mbali na mji tuko hapa hapa mjini tumejipanga kuhakikisha kombe linabaki Kaskazini na kutimiza malengo ya kwenda kimataifa" amesema Tito.

Amesema wamedhamiria kulipa kisasi kwa kuwafunga Yanga ambao waliwatumia kama ngazi kujitangazia ubingwa wa ligi Kuu Bara msimu huu 2021/22 Juni 15 katika uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kuwachapa mabao 3-0.

Ameongeza kuwa morali na hamasa iko juu wanategemea sapoti ya mashabiki wengi wa soka kutoka katika mikoa yote ya Kanda ya kaskazini kwa maana ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo wanatamani kuona timu yao inabeba ubingwa wa ASFC na kwenda Kimataifa.


Post a Comment

0 Comments