Ticker

6/recent/ticker-posts

Simba Sc Imevuna TSh1.1 Bilioni Msimu Huu

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Simba Sc Imevuna TSh1.1 Bilioni Msimu Huu

SIMBA imeshindwa kutimiza malengo iliyojiwekea msimu huu ambao ni kutetea ngao ya jamii, taji la Ligi Kuu, taji la Shirikisho la Azam (ASFC) pamoja na kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya klabu Afrika lakini pamoja na hayo imemaliza msimu huku akaunti yake ikiwa imenona kwa fedha.

Kwa kujihakikishia kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, Simba msimu huu imemaliza ikiwa imevuna kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya Sh1.1 bilioni kutokana na zawadi za mashindano tofauti ambayo imeshiriki.

Kiasi kikubwa cha fedha ambacho Simba imevuna msimu huu ni kile ilichokipata kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika Dola 350,000 (Sh816 milioni).

Ukiondoa fedha hizo kutoka CAF, Simba pia ina uhakika wa kuzoa Sh250 milioni kutoka Azam Media kama fedha za bonasi za kumaliza katika nafasi ya pili, kwa mujibu wa mkataba wa udhamini wa haki za matangazo ya Ligi Kuu baina ya kampuni hiyo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania.

Pia Simba imekusanya Sh50 milioni kutoka kwa mdhamini wao mkuu, Kampuni ya Sportpesa kama zawadi ya kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Fedha nyingine ambayo Simba imepata ni ile ya ubingwa wa Kombe la Mapinduzi Sh25 milioni, pia itapata fedha za ushindi wa pili wa Ligi Kuu, kiasi ambacho bado hakijawekwa hadharani ingawa inafahamika bingwa anapata kitita cha Sh100 milioni ambaye ni Yanga.

Hata hivyo, kiasi hicho cha fedha ambacho Simba imekipata msimu huu kama zawadi za kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali, kimezidiwa na kile ilichokipata msimu uliopita ambao ilifanya vizuri sana.

Simba katika msimu uliopita, ilipata Dola 650,000 (Sh1.5 bilioni) kutoka CAF kwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikapata Sh100 kutoka Sportpesa kama pongezi kwa kutinga hatua hiyo na kutwaa ubingwa wa ligi kuu.

Kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Simba ilipata Sh100 milioni na ikavuna Sh50 milioni kwa kuwa mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam.

Meneja habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kutotimiza malengo yao msimu huu kumewapa nguvu ya kujipanga zaidi ili warudishe mataji msimu ujao.

“Malengo yetu yalikuwa ni kutetea mataji yetu na kufika nusu fainali lakini kwa bahati mbaya hatujaweza kuyatimiza. 

Uongozi unajipanga vilivyo kuhakikisha msimu ujao tunarudisha heshima na mataji yetu na niwaahidi tu Wanasimba kuwa tutafanya usajili wa kishindo wa wachezaji ambao watatufanya tutimize malengo yetu,” alisema Ally.

Je,Unatafuta Ajira? Bofya hapa Kutuma Maombi


Post a Comment

0 Comments