Ticker

6/recent/ticker-posts

Leeds United Waitandika Liverpool Anfield

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KOCHA Jurgen Klopp ametaka waajiri wake Liverpool kuzinduka na kuacha kusuasua iwapo wana ndoto ya kusalia ndani ya nafasi nne-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu. 

Hii ni baada ya miamba hao wa soka ya Uingereza na bara Ulaya kupepetwa 2-1 na Leeds United ugani Anfield mnamo Jumamosi. Crysencio Summerville alifungia Leeds bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili na kuwatoa waajiri wake kwenye mduara wa vikosi vinavyochungulia macho hatari ya kuteremshwa ngazi ligini.

Kichapo hicho kilisaza Liverpool katika nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 16 sawa na Crystal Palace waliocharaza Southampton 1-0 uwanjani Selhurst Park.

Licha ya Liverpool kutandika mabingwa watetezi na viongozi wa EPL, Manchester City 1-0 mnamo Oktoba 16, 2022, miamba hao sasa wamepoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya vikosi vya chini kwenye jedwali la EPL. Walicharazwa na Nottingham Forest 1-0 ugani City Ground mnamo Oktoba 22, 2022 kabla ya chombo chao kuzamishwa na Leeds.

Liverpool walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-0 dhidi ya Ajax katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 26, 2022.

Rodrigo Moreno aliwaweka Leeds kifua mbele katika dakika ya nne kabla ya Mohamed Salah kusawazisha mambo dakika 10 baadaye. Summerville alifungia Leeds bao la ushindi katika dakika ya 89 baada ya kushirikiana vilivyo na Patrick Bamford aliyemtatiza pakubwa kipa Alisson Becker.

Liverpool sasa wamekuwa wa kwanza kufungwa bao katika mechi nane kati ya 12 zilizopita kwenye EPL msimu huu. Sasa matumaini ya kupigania taji la EPL muhula huu yanazidi kudidimia na Klopp amewawekea masogora wake malengo ya kukamilisha kampeni ndani ya orodha ya nne-bora.

Ushindi wa Leeds ulikuwa wao wa tatu kutokana na mechi 12 zilizopita za EPL na wa kwanza tangu Agosti 2022. Matokeo hayo yanatarajiwa kuwapa motisha zaidi ya kuvaana na Tottenham Hotspur na Manchester City katika mechi mbili kati ya tatu zijazo ligini.

Post a Comment

0 Comments