Ticker

6/recent/ticker-posts

Man-United Waanza Europa League Kwa Kichapo Kutoka Kwa Real Sociedad

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


KAMPENI ya Manchester United kwenye kipute cha Europa League msimu huu ilianza kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Real Sociedad ya Uhispania mnamo Alhamisi usiku ugani Old Trafford.

Mechi hiyo iliidhinishwa kutandazwa baada ya vinara wa Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) na wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) kushauriana na kuafikiana kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II.

Hakuna muziki ulioruhusiwa kupigwa uwanjani wakati wa mechi hiyo na wanasoka wa pande zote mbili walivalia utepe mweusi mikononi huku wakidumisha kimya cha dakika moja kwa heshima ya marehemu Malkia Elizabeth II.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Sociedad lilifumwa wavuni kupitia penalti ya Brais Mendez katika dakika ya 59 baada ya beki Lisandro Martinez kunawa mpira ndani ya kijisanduku.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza isiyokuwa ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa nyota Cristiano Ronaldo kucheza barani Ulaya tangu 2002 alipokuwa tineja kambini mwa Sporting Lisbon ya Ureno.

Bao lililofungwa na Ronaldo katika kipindi cha kwanza halikuhesabiwa na refa baada ya kubainika kwamba alicheka na wavu za wageni wao kutokana na krosi ya Diogo Dalot akiwa ameotea.

Ronaldo alipoteza pia nafasi kadhaa za wazi za kusawazishia Man-United waliomtegemea pakubwa ubunifu wa Bruno Fernandes katika safu yao ya kati.

Man-United watapambana na Sheriff Tiraspol ya Moldova katika pambano la pili la Europa League mnamo Septemba 15, 2022.

Hii ni mara ya kwanza kwa Real Sociedad kusajili ushindi dhidi ya timu ya Uingereza katika mashindano ya bara Ulaya na United ilikuwa haijapoteza katika mechi 18 za Europa League ugani Old Trafford kabla ya kichapi cha Alhamisi.

Kwingineko Arsenal ilisajili ushindi wa 2-1 dhidi ya FC Zurich katika mechi yao ya ufunguzi ya kundi A, kombe la Europa. 

Post a Comment

0 Comments