Ticker

6/recent/ticker-posts

Wachezaji Simba wapewa Masharti magumu

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KATIKA kuhakikisha inanufaika na wachezaji Augustine Okrah, Mohamed Ouattara na Moses Phiri ambao imewanasa kwa kutumia kiasi kikubwa cha fedha, Simba imeweka masharti magumu katika mikataba ya wachezaji hao jambo litakalowafanya wawe makini na wenye nidhamu ya hali ya juu nje na ndani ya uwanja.


Meneja Habari na mahusiano wa Simba, Ahmed Ally, alisema mikataba ya nyota hao imejikita katika kuwafanya wajitume kwa nguvu zote kuhakikisha wanaisadia timu lakini pia kuwajenga kinidhamu ya uwanjani na maisha yao ya kawaida kiujumla.

“Tuna masharti ya aina mbili ambayo wachezaji wetu tunawapa ambayo ni ya kiufundi na kinidhamu. Ya kiufundi kama ni mshambuliaji basi tunamwambia tunahitaji ufikishe malengo ya mabao kadhaa, na kama ni kiungo naye ana masharti yake, mwingine tunamwambia acheze mechi kadhaa msimu huu.” 

“Vile vile kuna masharti ya nidhamu, kwamba ukipatwa na kosa la kinidhamu tunakukata mshahara. Tulianza kulifanyia kazi katikati ya msimu uliopita na kila mchezaji anafahamu hiyo." 

“Pia kanuni za kinidhamu ambayo kila mchezaji anapaswa kusaini na wamesaini wote, ili kufahamu ni vitu gani wanapaswa kufanya na vipi hawapaswi kufanya,” alisema Ahmed.

katika mikataba ambayo nyota hao wa kigeni na wengine ambayo wamesaini, Simba wameweka sharti la mchezaji husika kucheza idadi ya mechi isiyopungua asilimia 60 vinginevyo kutakuwa na punguzo la mshahara.

Lakini pia utoaji wa bonasi kama ilivyokuwa hapo awali, utaendelea kufanywa kulingana na mchango na ufanisi wa mchezaji husika ambapo wale watakaokuwa wakicheza watapata fungu kubwa kulinganisha na wale ambao watakuwa watazamaji.

Kutakuwa pia na faini za fedha kwa wachezaji kuchelewa mazoezini, mechi au safari za ndani na nje ya nchi lakini pia vitendo vya utovu wa nidhamu kwa timu, viongozi, mashabiki, mamlaka za soka pamoja na wadhamini.

Ukiondoa hilo, Simba pia imeweka kipengele cha mauzo kwa mkataba wa kila mchezaji (buyout clause) ikilenga kupata kiasi kikubwa cha fedha iwapo nyota wake anahitajika na timu nyingine. Kwa wazawa kiasi cha chini cha kumsajili mchezaji wa Simba mwenye mkataba ni Dola 100,000 (Sh 233 milioni) wakati kwa wale wa kigeni, nyota ambaye unaweza kuvunja mkataba wake kwa dau dogo, utahitajika kutoa kiasi kisichopungua Dola 400,000 (Sh 933 milioni).

Ally alifafanua kuwa “Tumejiwekea mikakati ya kwamba mchezaji wetu anapopata ofa tunafanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili. Tunaangalia maslahi ya Simba itakayopata kwa kumuuza mchezaji na vile vile maslahi ya mchezaji atapata endapo atapata akiuzwa.”

Ahmed Ally alisema kuwa kambini kocha wao Zoran Maki anata mechi za kirafiki kati ya nne hadi tano na tayari wamecheza mechi moja dhidi ya Ismaily na kutoka sare.

Post a Comment

0 Comments