Ticker

6/recent/ticker-posts

Chris Mugalu: Ajipanga upya

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

STRAIKA wa Simba, Chris Mugalu ameelezea mambo mbalimbali hasa aliyokumbana nayo msimu uliopita na kushindwa kufunga bao hata moja.


Anasema sababu kubwa ni majeraha ya mara kwa mara aliyopata hadi kushindwa kucheza michezo mingi mfululizo.

“Hata mechi nilizokuwa uwanjani sikuwa sawa kwa maana ya utimamu wa mwili kwenye hali ya ushindani. Pengine ndio maana nilikutana na changamoto ya kugongana na mwenzangu uwanjani nil iumia tena,” anasema Mugalu.

“Sikupata nafasi ya kucheza mfululizo dakika nyingi jambo ambalo lilikuwa changamoto kwangu ndio maana kwenye mashindano mengine niliyopata muda wa kucheza nimefunga mabao.”

Anasema akiwa FC Lupopo ya DR Congo aliwahi kukutana na changamoto kama hiyo ya kucheza msimu mzima bila kufunga bao lolote kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.

Mugalu anasema msimu uliofuata alionyesha makali kwa kumaliza mfungaji bora wa msimu hadi kupata ofa za kuhitajika na timu nyingine mbalimbali ikiwemo FC Lusaka iliyofanikiwa kupata saini yake.

“Hali hii ya kutofunga hapa Tanzania sio kama nimependa, bali ni changamoto ya majeraha niliyokutana nayo mfululizo,” anasema.

Anasema klichomsumbua ni tatizo la nyama za nyuma ya paja kumuuma mara kwa mara kutokana na kupenda kucheza kwa nguvu kushindana na mabeki wa timu pinzani ili kuhakikisha anaisaidia timu yake au kufunga mabao.

“Nikipata muda wa kupumzika na matibabu mazuri huwa napona na kurejea haraka uwanjani, ila muda mwingine huwa zinanisumbua kama ilivyo wakati huu, lakini naamini nitakuwa sawa na kurudi kwenye ushindani,” anasema Mugalu aliyefunga mabao mawili kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Mugulu bado ni mchezaji wa Simba kwani ana mkataba, lakini amekuwa akihusishwa kuondoka ndani ya timu hiyo kutokana na ofa anazodaiwa kupata.

Hata hivyo, bado viongozi wa Simba wamegawanyika juu ya uwepo wake ndani ya klabu hiyo, kwani kuna wanaotaka aondoke na wengine wanatetea abaki wakiamini ni mchezaji mzuri hata kama msimu uliopita hakufunga bao lolote.

Mugalu anasema hana wasiwasi wowote na hatma yake ya msimu ujao kwani ni mchezaji wa Simba maana mkataba wake umebaki mwaka mmoja.

“Naamini katika uwezo wangu. Msimu ulioisha ni changamoto tu za majeraha hadi kushindwa kufanya vizuri, kama nikibaki hapa nitarudi kwenye makali yangu au nikiondoka nitaenda kuonyesha ubora huko.

“Maisha ya mchezaji soka ndio yalivyo unaweza kuwepo kwenye timu ama ukaondoka. Hapo sina wasiwasi na lolote kati ya hayo mawili kuondoka ama kubaki, kwani naamini kwenye uwezo wangu.”

Inaelezwa mabosi wake wamepokea ofa tano kutoka timu mbalimbali zikitaka huduma yake zikiwamo Zesco United, Nkana Red Devils, Power Dynamos zote za Ligi Kuu ya Zambia na FC Saint-Eloi Lupopo ya Ligi Kuu ya DR Congo.

Akiizungumzia Simba, Mugalu anasema iko vizuri na itashangaza. “Ukiangalia msimu uliopita kuna maeneo tulishindwa kufanya vizuri pengine ilikuwa sababu ya kushindwa kufikia malengo tuliyojiwekea mwanzoni mwa msimu,” anasema.

“Tunakwenda kufanya maandalizi ya kutisha ili msimu ujao turudi katika ubora.”

Post a Comment

0 Comments