Ticker

6/recent/ticker-posts

Robertinho: Tunakwenda kupambana na Vipers SC tukiwa na matumaini ya kufanya vizuri

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amesema kikosi chake kimedhamiria kupambana hadi tone la mwisho na kuhakikisha kinashinda mchezo wa marudiano dhidi ya Mabingwa wa Uganda Vipers SC, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Hatua ya Makundi.

Simba SC itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumanne (Machi 07), ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Vipers SC iliyokuwa nyumbani Uganda.

Robertinho amesema anafahamu Vipers SC watakuja Dar es salaam kupambana zaidi ya ilivyokuwa mchezo uliopita, hivyo wanajiandaa kukabiliana nao, huku wakitanguliza lengo la kupata alama tatu katika Uwanja wa nyumbani.

Kocha huyo amesema: “Tunakwenda kupambana na Vipers SC tukiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri, hasa baada ya kupata ushindi katika Uwanja wa ugenini juma lililopita.”

“Vipers ni timu ngumu na yenye wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kutoa upinzani kwa timu yoyote, hilo tunalifahamu na tutawapa heshima kubwa wakija hapa, ila halitupotezei malengo ya kupambana na kupata ushindi katika Uwanja wa nyumbani.”

“Simba SC inahitaji kushinda michezo miwili ya hapa nyumbani, kwa hiyo kila mmoja katika Benchi langu la Ufundi na Wachezaji wote tunafahamu hilo ndio kusudio kubwa kwa sasa, kwa hiyo hatutabweteka zaidi ya kupambana.”

Vipers SC inayoshiriki kwa mara ya kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika inaburuza mkia wa Kundi C ikiwa na alama 01.

Kwa Upande wa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipers SC Roberto Luiz Bianch Pelliser amesema kikosi chake kitacheza dhidi ya Simba SC katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kikiwa na lengo la kutafuta ushindi, utakaowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Kundi C.

Kocha huyo kutoka nchini Brazil ambaye alijiunga na Vipers SC mapema mwezi Januari baada ya kuondoka kwa Kocha Robertinho aliyeibukia Simba SC, amesema anajuwa mchezo wa Jumanne utakuwa mgumu lakini amejipanga kuhakikisha wanapata ushindi.

“Ninatambua ukubwa na ugumu wa kucheza na Simba SC hasa wakiwa katika Uwanja wao wa nyumbani, lakini moja ya mikakati yangu ni kuona tunaweza kupata ushindi ili tujiweke katika nafasi nzuri na kufuzu Hatua ya Robo Fainali.”

“Tulipoteza mchezo wetu uliopita dhidi ya Simba SC tukiwa nyumbani Uganda, lakini nafasi ya kufanya vizuri ipo wazi kwetu kama Simba SC walivyofanya walipocheza ugenini, ingawa tuna jukumu kubwa la kupambana Dar es salaam.”

“Nimewasisitiza baadhi ya wachezjai wangu kuwa makini, kwa sababu Simba SC ina wachezaji wenye uzoefu na hatari, kwa hiyo tunaendelea kujiandaa na bado hatujakata tamaa ya kupambana na kumaliza katika nafasi nzuri katika kundi letu.” amesema Kocha Bianchi.

Katika msimamo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Raja Casablanca ya Morocco inaongoza msimamo wa Kundi C ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na Horoya AC ya Guinea yenye alama 04, Simba SC ipo nafasi ya tatu ikifisha alama 03 na Vipers SC ipo nafasi ya mwisho kwa kuwa na alama 01.

SIMBA YAJA NA ‘WENYE NCHI BEACH PARTY’

Post a Comment

0 Comments