Ticker

6/recent/ticker-posts

Robertinho: Chama, Saido watashangaza

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa



Kocha Mkuu wa Simba, Robert Oliviera ‘Robertinho amefanya mahojiano maalum na kufafanua mambo mengi ikiwemo mafanikio yake na mwenendo wa timu hiyo ikiwemo mastaa wake Chama na Saido.


Robertinho ameiongoza Simba kwenye michezo 10 ya mashindano akishinda 7, sare moja na kupoteza mbili. 


“Nimepata ushirikiano mkubwa ndani ya Simba kuanzia uongozi timu mpaka mashabiki, tunaishi kama familia mimi wachezaji wenzangu na wasaidizi wangu wote, kadri ya muda unavyokwenda tunazidi kuishi na kushikamana kama familia, utawala nao kila mmoja anafanya kazi yake kubwa kutoka kwao ni ushirikiano mkubwa ninaoupata.


“Wanaheshimu nafasi yangu na hilo ndio la msingi lakini kubwa zaidi ya yote ni mashabiki wetu siku zote wako nyuma yetu ni changamoto kwetu kuhakikisha tunafanya kazi vizuri ili tudumishe furaha yao,”anasema


“Kabla sijafanya uamuzi wa kuja Simba, nilikuwa na mtihani wa kuamua wapi kwa kwenda kupitia ofa kubwa nzuri tano mezani baada ya kuondoka Vipers,ofa hizi zilikuja kutokana na rekodi yangu kupitia mafanikio niliyoyapata hapa Afrika Mashariki.


“Nikiwa Rwanda na Rayon Sports nimeifundisha kwa miaka minne nikachukua mataji yasiyopungua matatu likiwemo ubingwa wa ligi, nilipotoka hapo nikaenda Uganda Vipers nako nikachukua mataji lakini kubwa hapa likawa kuifanya Vipers kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tena tukimng’oa TP Mazembe.


“Hatua hii ilioniongezea thamani kubwa na klabu mbalimbali kuhitaji huduma yangu, Simba ilikuwa moja ya klabu ambayo ilinitaka na sasa nipo hapa lakini kabla ya kufanya maamuzi haikuwa rahisi kutokana na ofa ambazo nilikuwa nazo, kuna moja ya Afrika Kusini, Tunisia,Misri lakini nikiwa nyumbani Brazil Simba wakatuma ofa yao nikaiangalia, nikaongea na familia yangu.


“Nakumbuka niliwahi kuja hapa nikiwa na Rayon Sport kwenye mchezo wa Cecafa, nilivutiwa na nilivyoingia uwanjani kuangalia mechi ya Simba nikaona uwanja karibu mzima mashabiki wameupamba kwa nguo za rangi nyekundu na nyeupe ile ilibaki ndani ya moyo wangu, niliipenda sana ile picha nikaona kwa ofa yao acha nije hapa.


“Nina furaha kuwa hapa hii ni klabu kubwa yenye kiu ya mafanikio, mashabiki wanaipenda klabu yao wakato wote wanatamani kuona timu inashinda lakini kubwa ni malengo ya uongozi wa klabu, unapokuwa nje unaiona Simba ni klabu kubwa lakini ukifika ndani unaiona kubwa zaidi.”


TOFAUTI YA VIPER NA SIMBA


Robertinho amefundisha soka Tunisia, Rwanda,Uganda na sasa hapa Tanzania akiwa na Simba anaeleza utofauti; “Kila nchi ina fikra zake zinazotofautiana lakini kitu muhimu unatakiwa kuwaelewa wachezaji wa Afrika, kwangu mimi sio kitu kigumu kwa kuwa huwa natumia uzoefu wangu wa kupitia kuwa mchezaji na sasa nikiwa kama kocha.”


“Unajua hata kwetu Wabrazil kuna wachezaji wenye asili ya Kiafrika tumecheza nao kwahiyo najua kujitofautisha na sehemu ninayokwenda, ukimjulia mchezaji unayemfundisha atakwenda kutoa uhai kukupigania uwanjani.


“Kokote ninakopita huwa sipendi kuwaongelea watu nyuma yao, maisha yangu napenda kama naona kitu kwa mchezaji namuita na nazungumza naye mimi na yeye, mimi ni kocha ambaye napenda kutoa mfano mzuri wa maisha kwa wachezaji wangu na wasaidizi wangu, sipendi kuwa mfano wa kuharibu nidhamu ya familia.


“Ni rahisi kwangu kukaa na mchezaji na kumuelewesha pale ninapoona hajachukua ninachofundisha kwa haraka, nitamwambia kwa ukarimu faida za kukaba au kuharakisha mashambulizi nitamueleza faida za kukaba kwa wenzake.


“Nitamwambia ukirudi kuja kusaidia wenzako sio lazima upokonye mpira lakini ziba lile eneo ambalo litakuwa wazi, nadhani hii imenisaidia hata hapa Simba sasa wachezaji wameelewa kwa haraka kile ninachotaka kifanyike.


“Soka sio kipaji peke yake unaweza kukuta mchezaji ana kipaji na ujuzi anapokuwa uwanja wa mazoezi lakini anapokuja uwanjani mbele ya mashabiki akapoteza kujiamini kufanya kile ambacho alikuwa anakifanya mazoezini.


“Hiki ndio kwa haraka nimekiona kwa baadhi ya wachezaji hapa unamuona mchezaji anafanya kitu kikubwa uwanja wa mazoezi lakini akija uwanjani anajaa presha anapoteza kujiamini nadhani wachezaji wengi wanapaswa kujijenga kwenye hili, kazi yangu kama kocha ni kumjenga mchezaji wa namna hii kumsaidia azoee presha ya mashabiki.



CHAMA, SAIDO WATASHANGAZA


Wakati Robertinho anatua Simba changamoto kubwa ilikuwa kwa wachezaji wake baadhi mastaa kuingia katika mifumo yake na sasa amekiri kwamba kuna mengi makubwa watayafanya mastaa wake na yatashangaza uwanjani kwani wanajua.


“Nipo hapa Simba kwa miezi mitatu sasa, nadhani lilikuwa ni suala la muda tu nikuulize swali angalia wakati nafika na sasa hali ikoje, nadhani wachezaji wangu ni prefeshno sana wamebadilika kwa idadi kubwa,hili lilikuwa jukumu langu kuhakikisha ninachotaka kifanyike kinaelewa na kifanikiwa. “Hebu muangalie Chama (Clatous) sasa, muangalie Saido (Ntibazonkiza) pia, muangalie Yassin (Mzamiru),Kapombe (Shomari),unamuonaje Tshabalala (Mohamed Hussein),vipi Inonga (Ennock).


“Nitakupa mfano muangalieni Nyoni anavyoingia kipindi cha pili,tukiwa kule Uganda tukicheza na Vipers, tulikuwa tunaongoza kwa bao moja, kipindi cha pili wapinzani wetu walikuja na nguvu sana walitushambulia sana.


“Watu wengi wakaanza kusema kwa kupiga kelele wanasema tuingize mshambuliaji mwingine nikawaza nikasema hapana hapa tunahitaji kiungo mwingine mkabaji kuja kuongeza nguvu nikamuinua Nyoni (Erasto) nikamuita nikampa maelekezo.


“Alipoingia baada ya muda tukawa tumeweka mizani sawa wa majukumu ghafla tukawatuliza Vipers ilikuwa tuwapige bao la pili lakini kikubwa tulilinda vizuri bao letu kwa kazi kubwa aliyoifanya Nyoni. Ni mtu sahihi kwetu tunapotaka mtu wa kuongeza nguvu kwenye ulinzi anajua kucheza kwa nidhamu ya mchezo.


“Soka ni mchezo unaochezwa kwa kusaidiana hakuna mchezaji anayeweza kucheza mpira peke yake, sasa timu inacheza kama familia hiki ndio kitu nilikuwa nakihitaji na ndio maisha yetu ndani ya Simba sasa.

Uongozi Simba wahaidi makubwa mechi dhidi ya Raja Casablanca

Post a Comment

0 Comments