Ticker

6/recent/ticker-posts

Makocha Yanga, Simba kila mmoja atamba kuibuka na ushindi

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


"MCHEZO wa Ngao ya Jamii utakaopigwa leo makocha wa timu zote mbili Yanga na Simba kila mmoja ametamba  kuibuka na ushindi na kuondoka na taji hilo."

Katika mchezo huo mwamuzi wa kati atakuwa ni Heri Sasii, kutoka Dar es Salaam, akisaidiana na Mohamed Mkono kutoka Tanga na Kassim Mpanga (Dar es Salaam) na mwamuzi wa akiba ni Ramadhani Kayoko (Dar es Salaam). 

Akizungumza jana Kocha Mkuu wa Simba, Zoran Maki, alisema kuwa wamejiandaa vizuri kwani mchezo huo ni mkubwa ambao utaamuliwa na wachezaji wakubwa ingawa ni wa kawaida kama mingine.

“Mchezo ni dakika 90 timu yangu iko tayari kwa ajili ya mchezo tutashuhudia mechi nzuri na timu bora itapata  matokeo mazuri,” alisema Maki.

“Wachezaji wote wako vizuri ingawa tunaenda kumkosa Aishi Manula ambaye ana majeraha na hajafanya mazoezi na timu,” alisema Maki.

Nahodha wa Simba John Bocco, alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo ni mazuri wanaiheshimu Yanga, lakini kwa jinsi walivyojiandaa anaamini wanaenda kupata ushindi.

“Utakuwa mchezo mzuri tuna kikosi chenye wachezaji wazuri naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kwani mechi hii itaenda kutoa taswira yetu ya msimu ujao,” alisema Bocco.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi,  alisema kuwa utakuwa mchezo mzuri wa kiufundi utakaokuwa ukifuatiliwa zaidi barani Afrika ingawa umekuja mapema zaidi katika kipindi cha maandalizi ya msimu mpya.

“Namkaribisha kocha Zoran na namtakia kila la heri kwenye mchezo huu, lakini pia nina furaha kwa kuwa kocha niliyefikisha michezo sita ya watani wa jadi,” alisema Nabi.

“Tumejiandaa vizuri ingawa mchezo huu umekuja mapema wachezaji wako kwenye hali nzuri tunaenda kumkosa Lazarous Kambole, ambaye alipata majeraha kwenye mchezo wa Namungo pamoja na Moloko ambaye kesho (leo) hatakuwa sehemu ya kikosi.”

Nahodha wa Yanga, Bakari Nondo, alisema kuwa wao na benchi la ufundi wamejindaa vizuri kwa mchezo huo na anaamini wanaenda kutetea Ngao ya Jamii.

“Alisema kuwa matokeo yaliyopita hayawezi kuwatoa mchezoni na kuwataka mashabiki wa Yanga wajitokeze kwa wingi kwani wamepanga kuwashangaza,” alisema Nondo.

Mechi ya leo inatarajiwa kuwa kali ya kusisimua kutokana na aina ya usajili ambao timu zote zimeufanya, huku baadhi ya wachezaji wakicheza 'dabi' hiyo kwa mara ya kwanza.

Simba ndiyo inayotarajia kuingia uwanjani na kuchezesha wachezaji wengi wapya kutokana na mapungufu waliyokuwa nayo msimu uliopita, tofauti na Yanga ambayo itakuwa inaziba tu baadhi ya mapengo ya msimu uliopita, lakini kwa asilimia kubwa ikitegemea kikosi kilekile.

Simba itakuwa na wachezaji wapya kama Augustine Okra, Vicent Akpan, Nelson Okra, Mohamed Ouattara na wengineo, huku Yanga ikiwa na kina Lazrous Kambole, Aziz Ki, Joyce Lomalisa, Gael Bigirimana na wengine. 

Pia Yanga itakuwa na faida ya kuendelea kuwa na kocha wake wa msimu uliopita, Nabi wakati Simba ikiwa na kocha mpya, Maki mwenye uraia wa nchi za Ureno na Serbia.

Simba itataka kulipiza kisasi cha kufungwa kwenye Ngao ya Jamii msimu uliopita, ilipopata kipigo cha bao 1-0, Septemba 25 mwaka jana, likiwekwa wavuni na Fiston Mayele dakika ya 12 ya mchezo.

Tangu kuanza kwa Ngao ya Jamii, timu hizo zimekutana mara tano, Simba ikishinda mbili na Yanga mara tatu.

Mara ya kwanza ilikuwa ni 2001, Yanga ikishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Edibly Lunyamila na Ally Yusuph 'Tigana', huku bao la kufutia machozi la Simba likiwekwa wavuni na Steven Mapunda 'Garincha'.

2010 Yanga ilitwaa tena Ngao ya Jamii kwa kuifunga Simba kwa mikwaju 3-1 ya penalti, baada ya dakika 90 za suluhu, huku 2011, Simba ikishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Haruna Moshi 'Boban' na Felix Sunzu.

Simba ilifanikiwa ilichukua Ngao ya Jamii mbele ya Yanga 2017 kwa mikwaju 5-4 ya penalti, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka jana, Yanga ikishinda bao 1-0.


 

Post a Comment

0 Comments