Ticker

6/recent/ticker-posts

Sopu: Afunguka alivyozikacha ofa za Simba, Yanga

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

NYOTA mpya wa Azam FC, Abdul Suleiman ‘Sopu’ amevunja ukimya na kufunguka juu ya namna alivyokacha ofa za Simba na Yanga na kuamua kutua klabu hiyo ya Chamazi kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Azam na la Shirikisho Afrika.


Sopu alikuwa akiwindwa na klabu hizo kubwa nchini kutokana na kiwango alichoonyesha msimu uliopita hususan kwenye fainali ya ASFC kati ya iliyokuwa timu yake ya Coastal Union dhidi ya Yanga alipofunga hat trick iliyofanya pambano hilo lililopigwa dakika 120 kwisha kwa sare ya mabao 3-3 kabla ya Yanga kushinda kwa penalti 4-1.

Hata hivyo, Sopu aliyewahi kupita Simba aliamua kuzipotezea ofa hizo za vigogo na kutua Azam na mwenyewe amefichua ilivyokuwa ngumu kufanya uamuzi, ingawa anaamini mahali alipotua kwa sasa ni sehemu sahihi kwa kipaji chake.

Akihojiwa, Sopu alisema: “Zile ni timu kubwa, lakini Azam ni kubwa pia. Niliziona ofa zao ila niliamua kwenda Azam nikiamini ndio sehemu sahihi zaidi ya kucheza muda huu.”

“Haikuwa rahisi kwani wengi walitamani niende kule lakini binafsi nilifuata matakwa yangu na Azam ilinipa ushirikiano wa kutosha hadi naenda kusaini kila kitu kilikuwa tayari.”

Msimu uliopita Sopu, aliyepo kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars inayojiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za michuano ya wachezaji wa ndani ya Afrika (Chan) dhidi ya Somalia, alifunga jumla ya mabao 16, huku tisa yakiwa ya ASFC yaliyompa tuzo ya mfungaji bora na mchezaji bora wa michuano hiyo, huku katika ligi akitupia saba.

Post a Comment

0 Comments