Oct 21, 2016

Magufuli aagiza HESLB kukusanya madeni kwa kasi

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Magufuli ameagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kutumia Sheria zilizopo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni kwa wahitimu walionufaika na mikopo.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo jijini Dar es salaam wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa hosteli za wanachuo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unajengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa gharama ya shilingi bilioni 10.

Amesema kuwa Serikali inadai takribani shilingi trilioni 2.6 kwa wahitimu walionufaika na mikopo ya Elimu ya juu.

“Serikali inawadai wahitimu walionufaika na mikopo ya Elimu ya juu takribani shilingi trillion 2.6 ambazo wanatakiwa kuzirudisha ili ziweze kutolewa kama mikopo kwa wanafunzi wapya na waliopo vyuoni” alifafanua Dkt Magufuli.

Aidha Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kusimamia ipasavyo suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi kwa kuzingatia vigezo vilivyopo kwani lengo la mikopo hiyo inawalenga watoto maskini.

Alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya malalamiko ya kuwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya zoezi la ugawaji wa mikopo hiyo kwa upendeleo hivyo kuzitaka uongozi wa Wizara kushughulikia suala hilo.

Mbali na hayo Rais Magufuli amewataka wanufaika wa mikopo hiyo kutimia mikopo hilo kwa malengo mazuri katika kujinufaisha na masuala ya Elimu.

Naye Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa mradi wa ujenzi wa hosteli hizo utasaidia kuwahudumia wanafunzi 3,840 ambapo unatarajiwa kuisha mwishoni mwa mwezi Desemba 2016.

Katika hatua hiyo Prof. Ndalichako alisema kuwa wanafunzi waliodahiliwa kwa mwaka huu wapo 58,000 hivyo suala la wanafunzi 66,000 kukosa mikopo hiyo ni upotoshaji unaofanya na baadhi wa watu.

Mradi wa Ujenzi wa Hosteli za wanachuo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wenye majengo 20 kila jengo gorofa nne zenye vyumba 12 unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba mwaka huu.
Read More

Rais Magufuli Afunguka kuhusu mikopo Vyuoni

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 483 kwa mwaka huu kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu ambapo wanafunzi zaidi ya 118,000 watanufaika.

Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi la hostel za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo, Rais Magufuli amesema miongoni mwa hao watakaonufaika, wanafunzi 93,000 ni wanaoendelea na masomo na wanafunzi takribani 25,000 ni watakaoanza masomo mwaka huu huku akiweka bayana kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia masikini.

Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji wa mikopo ikiwa ni pamoja na upangaji mbaya wa wanafunzi katika vyuo, kutoa mikopo kwa upendeleo, kutozingatia sifa za mkopaji, kutoa mikopo hewa na kufungua vyuo kabla ya mikopo ya wanafunzi kutolewa na pia amewaonya wanafunzi kujiepusha na vitendo visivyofaa wakati Serikali inarekebisha dosari hizo.

"Na ndio maana wakati mwingine na wabaya wanapitia humo humo, mara fanye hivi fanyeni vile, wakati wanajua kuwa mkifanya yasiyofaa Serikali itawafukuza tu ili mkafanyie mambo yenu huko.

"Kwa sababu huwezi kuwa unahangaika kutafuta fedha za kuwapa mikopo, wakati huo huo unahitaji kujenga reli, wakati huo huo unahitaji kujenga barabara, wakati huo huo unahitaji kulipa mishahara, wakati huo huo unahitaji kutoa elimu bure, wakati huo huo Karagwe kuna njaa, wakati huo huo watu wanahitaji dawa hospitali, halafu watu wengine wanataka kukuendesha kana kwamba hela unayokusanya ni kwa ajili yao tu, ni lazima tuelewane na mimi ninataka kuwaeleza kwa dhati lazima twende katika njia iliyonyooka, ni bora uwe Rais usiye maarufu lakini utimize uliyoyaahidi, asitokee mtu wa kukuendesha, ninajua mmenielewa" amesisitiza Dkt. Magufuli.

Dkt. Magufuli ameiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kujipanga vizuri kukusanya marejesho ya mikopo kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo ambapo mpaka sasa bodi inadai takribani Shilingi Trilioni 2.6.
Read More

Wanafunzi 66,500 waliokosa mikopo kufikiliwa Upya

KUNA matumaini mapya kwa wanafunzi 66,500 waliokosa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo ulioanza mwezi huu.

Matumaini hayo yanakuja baada ya kupatikana kwa habari kwamba Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii imeweka kwenye ratiba yake ya shughuli za kamati, suala la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Maelezo ya mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Zitto Kabwe aliyotoa jana kupitia mtandao mmoja wa kijamii ilisema "kamati itashughulia suala hilo kuanzia Jumatatu, kwa mujibu wa ratiba niliyoona."

"Natumai tutapata jawabu la wanafunzi walikosa mikopo."

Bodi ya Bodi ya Mikopo Elimu ya Juu (HESLB) ilitangaza juzi kuwa itatoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 tu kwa mwaka 2017/2017 hivyo kuacha 'vilio' kwa maelfu ya wanafunzi wanaotakiwa kusomea shahada katika vyuo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema juzi kuwa kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo hiyo, wanatarajia kutoa fedha hizo kwa 21,500 tu ambao "wamekidhi vigezo".

Kutokana na takwimu hizo, ni dhahiri wazazi ama walezi wa wanafunzi 66,500 watalazimika kuingia mifukoni kulipia gharama za elimu hiyo kwa watoto wao.

Aidha, mpaka sasa HESLB imetoa majina ya wanafunzi 3,966 ambao ni wanufaika wa kwanza wa mkopo kwa mwaka huu wa masomo.

Mwaka wa masomo uliopita bodi ilitoa Sh. bilioni 459 kwa wanafunzi 122,486, kati yao 53,618 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 68,916 ni waliokuwa wakiendelea na masomo yao.

Taarifa ya Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), ilisema zaidi kuwa "wajibu wa serikali yoyote duniani ni kuhakikisha kuwa watu wake wanapata elimu.

"Serikali inayoshindwa kusomesha watu wake haina haki ya kutawala."

Kamati ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii ipo chini ya uenyekiti wa Peter Serukamba ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CCM).

VIGEZO VIPYA
Akizungumzia vigezo vipya Badru alisema wanafunzi watakaopata mikopo hiyo ni wale waliokizi matakwa ya vigezo vipya vya mikopo vilivyotangazwa na serikali hivi karibuni.

Alisema wameanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea tangu juzi.

Alisema HESLB inatoa mikopo hiyo kulingana na kalenda za vyuo husika, na kwamba kwa juzi walitoa kwa vyuo vikuu vilivyokwisha fungua kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alisema hali ya kifedha katika HESLB ni nzuri na wanafunzi wapatao 21,500 wanatarajia kunufaika na mikopo.

“Siyo kila mwanafunzi aliyedahiliwa anaweza kupata mkopo, wengine wamedahiliwa lakini wanauwezo wa kujisomesha, hivyo tutatumia vigezo mbalimbali katika kutoka mikopo,” alisema Badru.

Mbali na UDSM, Badru alisema vyuo vingine ambavyo kwa awamu ya kwanza vimepata fedha ni pamoja na Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco), Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agustino (Saut), Chuo Kikuu cha Mzumbe (Muse), Chuo Kikuu cha Ardhi, Taaisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Hata hivyo, Ofisa Mikopo wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, Wilfred Medadi alisema hadi kufikia juzi walikuwa hawajapokea fedha zozote kutoka HESLB.

Alisema Jumanne chuo kilipokea fedha za ada za wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu za mwaka jana, na kwamba taarifa za wanafunzi wanaoendelea na masomo bado hazijarudishwa chuoni hapo kutoka HESLB.
Read More

Ukosefu wa dawa waibua hofu nchini

NI hofu na vilio kila kona sekta ya afya nchini kutokana na wagonjwa wanaofika katika hospitali mbalimbali kwa matibabu kukosa dawa.

Hatua ya kukosekana kwa dawa na vifaa tiba muhimu katika vituo vya kutolea huduma vya umma nchini, kumeelezwa kuathiri zaidi wananchi wasio na bima za afya na wale wenye bima zenye wigo mdogo.

Ukosefu huo wa dawa kwa sasa umekuwa mkubwa, hali inayotishia kutokuwapo uhakika wa huduma kwa wagonjwa katika vituo vya afya.

Kwa mujibu wa takwimu, inaelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi hawamo katika mfumo wowote wa bima za afya, na inapotokea uhaba wa dawa na vifaa tiba, hujikuta wakiathirika zaidi kwani hulazimika kutumia gharama kubwa kupata huduma, na wakati mwingine hukosa kabisa.

Imeripotiwa kuwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imefikia hatua ya kutoagiza dawa kama njia ya kulinda mtaji wake ambao umekuwa ukizidi kutetereka kutokana na madeni yanayozidi kulimbikizwa serikalini pamoja na vituo vya kutolea huduma.

Baadhi ya hospitali zilizokumbwa na kadhia ya kukosa huduma MSD, ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, hospitali za wilaya za Kiteto, Mpwapwa na nyingine nyingi.

Kwa mujibu wa uchunguzi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa na MSD zaidi ya Sh bilioni 90.

Baadhi ya hospitali zinazodaiwa na MSD ni Muhimbili (Sh bilioni 8) na Hospitali ya Wilaya ya Kiteto (Sh milioni 38). 

SERIKALI
Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais Samia alikiri kuwapo uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za Serikali nchini.

Alisema hata hivyo uhaba wa dawa nchini ni changamoto ya muda mfupi kwani Serikali inatafuta ufumbuzi wa haraka kuwahudumia wananchi.

Samia alitoa kauli hiyo siku chache baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kusema hakuna uhaba wa dawa nchini.

“Tumetenga bilioni 70/- kwa ajili ya kumaliza tatizo la dawa nchini, pia tumetenga jumla ya Sh bilioni 85 kwa ajili ya kupunguza deni MSD. Nia yetu ni kutaka huduma za afya ziwe zenye ubora,’’ alisema.

Samia alisema Serikali ina mpango wa kujenga kiwanda cha dawa katika Mkoa wa Simiyu ili kuweza kukabiliana na tatizo la dawa hapa nchini.

Alisema kuwa changamoto hiyo ni ya mpito huku akizitaka hospitali nchini kukusanya mapato yao ambayo yatasaidia ununuzi wa dawa.
Read More

Wanafunzi vyuo vikuu walia njaa nchi nzima

WANAFUNZI vyuo vikuu nchi nzima wanalia njaa kutokana na kupunguziwa fedha za kujikimu.

Hali hiyo, imedhihirika baada ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), kulalamikia uamuzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB) kupunguza kiasi cha fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Sh 510,000 hadi 19,000 kila baada ya miezi miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(DARUSO), Erasmi Leon, alisema kiasi cha fedha kilichotolewa mwaka huu ni kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Leon alikutana na waandishi wa habari baada ya kufika Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa lengo la kutaka kuonana na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ili waweze kumweleza malalamiko yao.

Alisema hali hiyo inaweza kuwasababishia wanafunzi kuishi maisha magumu na kushindwa kufanya vizuri darasani.

Alisema wanafunzi hao, pia wamepewa Sh 7,322 kwa ajili ya gharama za stationary na vitabu wakati kipindi kilichopita walikuwa wakipewa Sh 200,000 kwa mwaka.

Alisema licha ya kupewa fedha hizo, idadi ya wanafunzi walioomba mikopo katika chuo hicho kwa mwaka huu ni zaidi ya 5,000, waliobahatika kupata mikopo hiyo ni wanafunzi 949.

“Kiasi cha fedha za mikopo kilichotolewa mwaka huu ni kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita, jambo ambalo linaweza kusababisha wanafunzi kuishi mazingira magumu ya kutangatanga na wanafunzi wakike kuanza kujiuza,”alisema Leon.

Alisema Serikali ilipaswa kushirikisha wadau mbalimbali katika mfumo wa utambuzi wa kupata majina ya wanaostairi kupewa mikopo na kwa kiasi gani (mean tested) ili waweze kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo.

Alisema, mfumo wa utambuzi ambao pia unahusisha mambo mawili ambayo ni pamoja na ada pamoja na vitivo maalumu,ungeweza kuzingatia vigezo vya utoaji wa utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi hao.

“Hebu fikiria kama Serikali imetoa Sh 19,000 kwa ajili ya chakula, usafiri na hiyo hiyo pia inatakiwa itumike kwa makazi, unaweza kuitumia kiasi gani ili iweze kukidhi mahitaji,?, serikali ilipaswa kuangalia upya suala hilo kabla ya kuamua kutoa mikopo,”alisema Leon.

Aliongeza, serikali ya wanafunzi imewasiliana na viongozi wa wizara ili kuzungumzia suala hilo lakini wameambia linafanyiwa kazi.

Aliwataka wanafunzi kutosaini fedha hizo kwa madai kuwa, hakuna sababu ya kuchukua fedha hizo wakati haziwezi kukidhi mahitaji.

“Ni bora kukosa fedha kabisa, kuliko kupata kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi, Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa umakini zaidi,”alisema.

Alisema baadhi ya wanafunzi wametoka mikoani ambao wanaweza kushindwa kwenda chuo kutokana na ukosefu wa fedha na kujikuta wanaishia mitaani kwa ajili ya kutafuta fedha.

TAHLISO
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Shrikikisho la Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO),Stanslaus Kadugalize alisema tatizo la utoaji wa fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu, limefikishwa kwenye bodi na kwamba upangaji utafanyika upya baada ya uliopo kuonekana kuwa na dosari.

Alisema upangaji wa sasa ulifanyika kwa kuangalia asilimia ya mkopo aliopata mwanafunzi suala lililosababisha wenye asilimia ndogo kupata kiasi kidogo.

Alisema upangaji huo umeathiri wanafunzi wa mwaka wa kwanza tu na kwamba upangaji mpya wa fedha hizo utatolewa Jumatatu ijayo.

“Ni vyema wanafunzi wavute subira kwa sababu tumeshakutana na Bodi ya Mikopo pamoja na Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi, Sayansi na Teknolojia na tumekubaliana kuwa upangaji ufanywe upya na kufikia Jumatatu ijayo utakuwa umekamilika,” alisema Kadugalize
Read More

Habari Katika Magazeti Ya Leo Ijumaa ya Octoba 21


Read More

TBS Kufumuliwa..... Waziri Asema Litaundwa Upya, Vijana wapya Kuajiriwa

WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema atalifumua na kuliunda upya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kwamba wameshaanza kutafuta vijana 136 watakaoajiriwa katika shirika hilo kwa lengo la kudhibiti bidhaa, zinazoingizwa nchini chini ya viwango.

Aidha, wataweka kitengo maalumu kwa vijana hao, watakaokuwa na uwezo wa kuchunguza mipaka ya nchi, kunusanusa katika bandari bubu, kukamata, kuwasiliana na Polisi na kusimama mahakamani kutoa ushahidi.

Mwijage aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati wa utoaji wa tuzo kwa washiriki wa Programu ya Kaizen iliyo chini ya Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Alisema lengo la kuiunda upya TBS ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika ipasavyo ili kulinda viwanda vya ndani, vinavyozalisha bidhaa mbalimbali.

“Tutahakikisha kwamba hakuna bidhaa zitakazoingia bandarini bila ya kuwa na viwango vinavyotakiwa. Lengo ni kuwalinda walaji na viwanda vyetu, kwa nini tuagize vitu nje wakati viwanda vyetu vinazalisha bidhaa,’’ alisema Mwijage.

Hatua yake hiyo imekuja siku chache, baada ya makontena 100 kutoroshwa katika bandari kavu za Dar es Salaam bila ya kukaguliwa na hivyo kuikosesha mapato serikali na pia kuwa na hatari ya kuingiza bidhaa zilizo chini ya kiwango.

Akizungumza utekelezaji wa agizo la Mwijage na hadi Jumanne wiki hii kwa waliotorosha makontena hayo kujisalimisha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Egid Mubofu alisema jana kuwa waziri ameongeza siku za utekelezaji wa agizo lake la kuwataka wafanyabiashara walioingiza maontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, watoe taarifa.

Dk Mubofu alisema baada ya agizo la awali, lililokuwa linamalizika Jumanne Oktoba 18, waziri aliongeza hadi leo ndipo hatua stahiki zichukuliwe.

Hata hivyo, alisema mwitikio umekuwa mkubwa na baada ya majumuisho ya leo, atakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa taarifa kuhusu suala hilo. 

Septemba 13, Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika hilo.

Mwijage alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.

Akizungumzia Programu ya Kaizen, Waziri Mwijage alisema jambo linalotakiwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba viwanda vingi, vinakuwa na mfumo huo wa Kaizen, kwani utasaidia kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya hali ya juu.

Alisisitiza lazima wafanyabiashara waboreshe bidhaa zao na kwamba wasitengeneze bidhaa kumtosheleza mteja bali kumridhisha mteja.

“Hatutaki kuingiziwa bidhaa ‘midabwada’ wala mataputapu, tunachotaka ni bidhaa zenye viwango vinavyotakiwa na tunataka wazalishaji wetu mzalishe bidhaa zenye viwango na viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuuza nje ya nchi,’’ alifafanua.

Hata hivyo, alisema sababu ya viwanda kufa ni baada ya kufunguliwa milango ya bidhaa kutoka nje kuingia nchini, ambazo hazikukidhi viwango na kwamba wafanyabiashara kutoka nje walikuwa wanashindana na wafanyabiashara waliopo, ambao waliwekeza fedha nyingi katika miradi yao.

Kwa mujibu wa Mwijage, mpango huo wa Kaizen umefanywa katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma ambapo umesaidia kuongeza tija katika uzalishaji na kupunguza upotevu wa malighafi.

Aidha, aliwataka Watanzania kupenda vitu vya nyumbani kwani wanahakikishiwa ubora na endapo vitakuwa na tatizo ni rahisi kuwabana wafanyabiashara wa ndani kuliko wa nje.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa JICA nchini, Toshio Nagase alisema mpango huo umesaidia kufundisha wakufunzi kwenye kampuni na viwanda zaidi ya 50 vilivyopo nchini.

Nagase alisema Kaizen imeleta matokeo kwa vitendo kwenye maeneo ya biashara kwa njia ya kusafisha eneo, kupunguza malighafi, kuhakikisha ubora wa bidhaa na kubadilisha tabia au motisha kwa wafanyakazi.

‘’Tunaamini kwamba Kaizen ni jambo muhimu katika kutengeneza viwanda vyenye ushindani kibiashara na kufanikisha lengo la kukuza viwanda kuelekea mwaka 2025,’’ alisema.

Alisisitiza kuwa mradi huo wa miaka mitatu, ulianza mwaka 2013 na kwamba ulianza Japan na nchi za Afrika unatekelezwa katika nchi za Ethiopia, Tunisia, Misri, Ghana, Zambia na Tanzania
Read More

Majambazi wawili Wauawa..... Bunduki 9 Zakamatwa

Jeshi la polisi limedai kwamba limeua majambazi wawili hatari na kukamata bunduki tisa, kati ya hizo SMG saba, shotgun moja na riffle moja, risasi 473 na magazini 16 baada ya majibizano ya risasi katika misitu ya Milima ya Usambara, Kijiji cha Magamba wilayani Lushoto. 

Katika majibizano hayo, pia polisi walidai kukamata bendera zenye maandishi ya lugha ya Kiarabu, redio saba za upepo na soksi za kuficha nyuso. 

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani alisema jana kuwa hiyo ilikuwa operesheni ya kuwasaka majambazi waliovamia Chuo Kikuu cha Sekomu, wilayani humo hivi karibuni.

Alisema katika tukio hilo, askari wawili walijeruhiwa kwa risasi. Marijani ambaye alikuwa katika milima hiyo inayodaiwa kuwa ngome ya majambazi hao, aliwataja waliouawa kuwa ni Mudrick Abdi (24) maarufu kwa jina la Osama, mkazi wa Mbagala Majimatitu Dar es Salaam na Sultan Abdallah (24) mkazi wa Kiembesamaki, Zanzibar. 

Alisema askari waliojeruhiwa wanaendelea na matibabu na kwamba hawakupata madhara makubwa kwa kuwa walikuwa wamevaa majaketi ya kuzuia kupenya risasi .
Read More