Ticker

6/recent/ticker-posts

Robertinho amaliza kazi Simba Afyeka na kutaja majembe anayotaka

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

BODI ya Wakurugenzi ya Simba imekabidhi majukumu ya usukaji kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao kwa Kocha Mkuu, Robertinho Oliveira Pamoja na wataalamu wengine wa mambo ya usajili na tayari shughuli imeanza kwa kufikishiwa majina ya wachezaji anaowataka. 

Simba imedhamiria kusuka kikosi imara kuelekea msimu mpya hususan kwa ajili ya michuano ya Super League, ikiwa ni timu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki itakayoshiriki kipute hicho kinachotarajiwa kushirikisha klabu kubwa nane barani Afrika kuanzia Oktoba mwaka huu.

Habari Kubwa Za Magazeti Ya Leo May 17, 2023

Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah (Try Again) amesema tayari Robertinho ameshapendekeza nafasi na majina ya wachezaji wapya ambao anawahitaji kwa msimu ujao ili kuimarisha timu hiyo kuwa na kikosi imara.

Alisema wamempa jukumu la usajili Robertinho ambaye atashirikiana na wataalamu wengine wa mambo ya usajili kufanya kazi hiyo ikiwamo kuangalia wachezaji wanaostahili kubaki kikosini na kupendekeza wapya wanaomfaa kulingana na mfumo wake jambo ambalo tayari amelifanyia kazi katika ripoti yake ya awali.

“Kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na maingizo mapya ya wachezaji msimu ujao, wenye maono ya kutufikisha pazuri katika michuano ya kimataifa, lakini kwa sasa kazi kubwa ni kuboresha na kuongezea mikataba kwa wachezaji wetu ambao wanatakiwa kusalia ndani ya kikosi cha msimu ujao,” alisema Try Again.

Alisema baada ya kutopata taji lolote msimu huu wamedhamiria kufanya maamuzi magumu katika mabadiliko ya kikosi chao kwa kusajili wachezaji ambao wataifikisha Simba katika malengo yanayotarajiwa na mashabiki.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kama bodi kwanza tutaangalia tathmini na ripoti ya kocha kwa viwango vya wachezaji, lakini jukumu la usajili mpya tayari mwalimu amefanyia kazi na kuleta maji au nafasi ya watu wake anaotaka kufanya nao kazi kwa msimu ujao,” alisema Try Again. 

Alisema wako katika kuboresha kikosi kwa sababu wanahitaji kufanya vizuri zaidi katika michuano ya msimu ujao ikiwamo Super League ambayo Simba imekuwa ni timu pekee kwa Ukanda wa CECAFA kushiriki kombe hilo la timu nane kubwa Afrika.

Wakati huo huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, aliwataka mashabiki kuachana na taarifa za nyota wao watatu muhimu, Clatous Chama,  Aishi Manula na Mohammed Hussein 'Tshabalala' kuwa hawatakuwa sehemu ya kikosi chao msimu ujao.

Alisema kulingana na ukubwa na wachezaji wazuri waliopo ndani ya Simba mashabiki wao watasikia mambo mengi kuhusu baadhi ya nyota kutakiwa kuondoka au kusajiliwa na klabu zingine.

“Hakuna ukweli juu ya nyota hao, tunatambua Manula aliumia na yuko kwenye matitabu, Chama na Tshabalala bado wataendelea kuonekana uwanjani, mashabiki wanapaswa kuelekeza nguvu katika mechi mbili zilizosalia kwenye ligi kuliko hizi taarifa za kututoa katika mstari,” alisema Ahmed. 

Aliongeza kuwa nyota hao wawili wako katika kikosi cha Simba na wanaendelea na maandalizi ya michezo miwili iliyosalia ya Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania utakaopigwa Mei 24, katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kabla ya kuhitimisha msimu uwanjani hao dhidi ya Coastal Union Mei 28, mwaka huu. 

Post a Comment

0 Comments