Ticker

6/recent/ticker-posts

Yanga yaahidi furaha congo

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KUELEKEA mchezo wa leo hatua ya makundi, mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele, amewahakikishia furaha mashabiki wa timu hiyo kwa kusema wamejiandaa kushinda dhidi ya Tp Mazembe katika mechi ya kukamilisha ratiba ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa mjini Lubumbashi, DRC.

Mayele amesema licha ya Congo ni nyumbani kwao, lakini kazi iliyompeleka ni moja ambayo ni kuitumikia Yanga na kufikia malengo ya kuvuna alama tatu muhimu.


Mayele alisema wanahitaji kupata ushindi katika mechi hiyo na kuonyesha ubora wa kikosi chao pamoja na kumfurahisha mdhamini wao Gharib Said (GSM) ambaye ameambatana na timu huko Lubumbashi.


“Bosi wangu amekuja katika ardhi ya nyumbani kwangu, anahitaji kupata furaha katika mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe, timu kubwa kwa hapa Congo lakini Yanga ni kubwa Tanzania, malengo yetu ni kusaka pointi tatu muhimu katika mchezo wetu wa Jumapili.


Sasa tunataka kushinda mechi hii ili kuonyesha ukubwa wa Yanga katika michuano ya kimataifa, nimewaahidi mashabiki kutetema katika uwanja uliopo nyumbani kwangu" alisema mshambuliaji huyo mwenye mabao matatu katika hatua ya makundi.


Aliongeza benchi la ufundi limefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita na sasa kazi kubwa imebaki kwa wachezaji kupambana kutafuta matokeo chanya ili kumaliza wakiwa kinara kwenye kundi lao.


Doumbia afunguka kinachomkwamisha Yanga

Naye Meneja wa Yanga, Walter Harryson, aliliambia gazeti hili kikosi chao kiko vizuri na wamekwenda Congo kwa lengo la kusaka ushindi.


Meneja huyo alisema maandalizi yote kuelekea mchezo huo yanakwenda vyema na wao wanatambua umuhimu wa kupata pointi tatu na hatimaye kujiweka imara kwa hatua inayofuata.


"Kikosi kiko katika hali nzuri kuhakikisha tunapata pointi tatu na kujiweka kwenye nafasi nzuri kuelekea hatua ya robo fainali, mchezo huu tunauhitaji kwa malengo makubwa, tunajua na tunatambua mashabiki wetu wanaosafiri na walioko hapa Congo wanahitaji ushindi," alisema meneja huyo.


Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, ametamba kikosi chao kiko kamili kusaka ushindi na kuendeleza shangwe lao la kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa.


Kamwe alisema wanajisikia fahari kuona timu yao imepata mafanikio makubwa katika msimu huu.


"Tunaongoza katika hatua ya makundi, tunaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, tumefuzu hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika," alitamba Kamwe.


Yanga inaongoza katika msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi 10 sawa na US Monastir ya Tunisia, Real Bamako ya Mali inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano wakati mabingwa hao wa zamani wa Afrika, TP Mazembe wanaburuta mkia wakiwa na pointi tatu.


Baada ya kumaliza mechi hiyo, Yanga itarejea nyumbani kujiandaa kuwakaribisha Geita Gold FC kwa ajili ya mechi ya hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA itakayochezwa Aprili 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments