Ticker

6/recent/ticker-posts

YANGA yausogelea ubingwa ligi kuu bara

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


YANGA imeendelea kuusogelea ubingwa wa ligi kuu bara baada ya ushindi wa bao 3-1 dhidi Geita Gold na kufikisha pointi 65 ikijichimbia kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya pointi nane na Simba iliyo nafasi ya pili.

Katika mechi hiyo, Geita ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 20 kupitia kwa mshambuliaji wake Elias Maguli lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Yanga ilirejea uwanjani kwenye kipindi cha pili kwa kasi na kupata mabao mawili ya haraka haraka dakika ya 49 na 50 kupitia kwa washambuliaji wake Kennedy Musonda na Clement Mzize huku Jesus Moloko akipachika la tatu dakika ya 70.

Clement mzize Azidi Kumkosha Nabi

Tangu Geita imepanda Ligi Kuu msimu uliopita haijawahi kupata ushindi wala sare kwa Yanga bali imechapwa mechi zote za ligi.

Bao la Maguli ni la kwanza kwa Geita kuifunga Yanga kwenye Ligi Kuu tangu matajiri hao wa dhahabu kupanda kutokea Championship msimu uliopita kwani kabla ya leo timu hizo zilikutana mara tatu na Yanga kushinda zote kwa ushindi wa bao 1-0.

Bao la Maguli ni la nne kwa upande wake tangu amejiunga na Geita katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, 2023 huku lile la Musonda wa Yanga likiwa la kwanza kwake kwenye ligi tangu ametua kwa Wanajangwani hao mwezi Januari akitokea Power Dynamo ya kwao Zambia.

Licha ya kuwa bao la Mzize ni la tano kwake kwenye ligi msimu huu lakini pia ni bao la kwanza la mchezaji mzawa wa Yanga kuifunga Geita kwenye ligi.

Kabla ya leo, mabao matatu iliyokuwa imeyapata Yanga dhidi ya Geita kwenye mechi tatu za ligi yalifungwa na wageni, Wakongomani, Jesus Moloko, Fiston Mayele na Mghana Benard Morrison.

Yanga ikishinda mechi nne kati ya sita zilizobaki itafikisha pointi 77 na kuwa Bingwa kwani Simba ambayo inamfukuzia kwa karibu ikishinda mechi zake sita zilizobaki itafikisha pointi 75 tu.

Ikumbukwe katika mechi zilizobaki, Yanga na Simba zitakutana April 16, mwaka huu.

Mechi sita za Yanga zilizosalia ni dhidi ya Kagera Sugar, Simba, Singida Big Stars, Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons.

Geita yenye pointi 34, nafasi ya tano kwenye msimamo imebakiza mechi tano dhidi ya KMC, Tanzania Prisons, Mbeya City, Ihefu na Mtibwa.

Post a Comment

0 Comments