Ticker

6/recent/ticker-posts

Yanga Yaanika Mkakati Mzima Wa Makombe, Robo Fainali CAF

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Uongozi wa Klabu ya Yanga umesema dhamira yao msimu huu ni kuhakikisha wanafanya makubwa kwenye michuano ya kimataifa na kuendelea kutetea mataji yaliyopo mbele yao.

Yanga kesho itashuka dimbani kwenye mchezo wa ASFC dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Baada ya mchezo huo wa kesho, Yanga itaanza kujiandaa dhidi ya Real Bamako ya Mali, ikiwa ni mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Saalam, baada ya Jumapili iliyopita timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.

Tayari kikosi cha Yanga kimeingia kambini jana, kujiandaa na michezo hiyo iliyopo mbele yao wakianza na Kombe la ASFC dhidi ya Tanzania Prisons. 

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema kikosi chao kipo tayari kwa ajili ya kwenda kutetea taji la ubingwa wa Kombe la ASFC kwa kuwakabili Tanzania Prisons.

Alisema dhamira kubwa ya Yanga ni kuhakikisha wanafanikiwa kutetea mataji yao yote, baada ya kuwa na uhakika wa Ligi Kuu Tanzania Bara na sasa wanalihitaji Kombe la ASFC.

“Mchezo wetu huo wa Tanzania Prisons na mingine ya Ligi Kuu tutatumia Uwanja wa Azam Complex, kutokana na Benjamin Mkapa kuwa kwenye ukarabati.

"Kuhusu mechi yetu ya kimataifa ya Jumatano ijayo, tutacheza katika Uwanja wa Mkapa na hii mechi tumekabidhi kwa mashabiki na wanachama ili kuhakikisha wanajitokeza uwanjani kwa wingi,” alisema Kamwe.

Alisema mechi yao dhidi ya Tanzania Prisons mbali na kutaka ushindi katika mchezo huo, lakini wanatumia kwa ajili ya maandalizi kuelekea mechi ya marudiano dhidi ya Real Bamako kuhakikisha wanapata pointi tatu.

Kamwe alisema mipango yao ni kuvuna pointi sita katika michezo ya kimataifa ambayo watacheza nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Michuano ya kimataifa tupo nafasi ya pili katika Kundi D tukiwa na pointi nne, ukipiga hesabu vizuri tiketi ya kucheza robo fainali imenyooka kwa asilimia 90 zinategemea pointi sita katika Uwanja wa Mkapa.

"Real Bamako kurudiana nao Uwanja wa Mkapa, tunaenda kutumia vizuri kupata ushindi katika mchezo huo pamoja kusaka alama zingine tatu za US Monastir jumla itakuwa 10, ambazo zitatufanya kufuzu na kucheza hatua inayofuata,” alisema Kamwe. 

Alisema siri kubwa ya kupata ushindi katika mchezo dhidi ya TP Mazembe ilichagizwa na hamasa za uwapo wa mashabiki wengi Uwanja wa Mkapa, hivyo akasisitiza kuendelea kujitokeza kwa wingi kuwahamasisha wachezaji wao.

“Kwa kuthamini mchango wa wanachama na mashabiki tumeamua hii mechi kuwakabidhi wao kujitokeza kwa wingi kufika uwanjani kwa ajili ya kushangilia mwanzo mwisho, ndio maana tukaipa Kaulimbiu ya 'Full Shangwe',  hiyo siku itakuwa ni shangwe tu Uwanja wa Benjamin Mkapa,” alisema Kamwe.

Post a Comment

0 Comments