Ticker

6/recent/ticker-posts

Uongozi Yanga Waipongeza Simba

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

 

Uongozi wa Yanga Chini ya Rais Injinia Hersi Said umewapongeza watani zao Simba kwa kushinda mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini dhidi ya Vipers Jumamosi iliyopita, huku nayo ikiahidi kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Akizungumza baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said, alisema tunawapongeza Simba kwa ushindi ugenini, lakini tunawapongeza wachezaji wetu wa Yanga na klabu nzima kwa sare ya ugenini ambayo naweza kusema, wote tulikuwa tunaelekea kupata pointi tatu, lakini ni mipango ya Mungu haikuwezekana.

"Nawapongeza wachezaji wetu kwa sababu huko ugenini hali haikuwa nzuri sana, hali ya hewa na mazingira ya ugenini, lakini tumeonyesha ni jinsi gani tuna kikosi imara ambacho kinaweza kupata matokeo sehemu yoyote na kwa hamasa hii namuahidi mheshimiwa siku ya tarehe nane tutakaporudiana na Real Bamako, sisi tutaendelea kupata matokeo mazuri," alisema Hersi.

Simba iliichapa Vipers bao 1-0 kwenye Uwanja wa St Mary's Chitende, Entebbe nchini Uganda, na Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa 26 Mars, Bamako nchini Mali, ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako, Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema pamoja na sare waliyoipata, haijawafanya kukata tamaa kwani kimahesabu timu yao ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye Kundi D la michuano hiyo.

"Tunamshukuru Mungu tuliondoka Dar es Salaam salama na leo kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu tumerejea nyumbani salama. Tumetoka Dar tukiwa na pointi tatu, tunarudi tukiwa na pointi nne kwenye kundi letu, maana yake kama klabu tumefanikiwa kuvuna pointi moja ugenini kwa hiyo hesabu zetu kwenye kundi letu bado zipo vizuri, niwaambie tu Yanga malengo yake ya kwanza makubwa mwaka huu ni kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho na kwa jinsi hesabu zilivyo kila kitu kipo sawa," alisema Kamwe.

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kwa niaba ya Rais Samia, aliipongeza Yanga, huku akizitaka timu za Tanzania kuendelea kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa na ahadi iko palepale.

Yanga  sasa inajiandaa na mechi ya Kombe la FA Ijumaa wiki hii dhidi ya Prisons.


Uongozi Yanga Watamba Kucheza Robo Fainali Kombe La Shirikisho Afrika

Post a Comment

0 Comments