Ticker

6/recent/ticker-posts

Robertinho Ameweka wazi kikosi cha FA Cup

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Kocha Mkuu wa Simba Robertinho ameweka wazi Kikosi kitakacho kushuka Uwanja wa Uhuru leo kuikaribisha African Sports kutoka Tanga kwenye mchezo wa hatua ya 16-bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) maarufu FA Cup.

Robertinho ameweka wazi wachezaji atakaowapa nafasi leo huku akimulika zaidi mechi ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers FC ya Uganda. 

Baada ya mchezo wa leo utakaopigwa saa 10:00 alasiri, Simba itaendelea na maandalizi yake ya mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers itakayopigwa Jumanne ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mchezo uliopigwa Uwanja wa St. Mary's nchini Uganda Jumamosi iliyopita, Simba ilishinda bao 1-0 shukrani kwa Henock Inonga, aliyeiwezesha kuvuna pointi tatu za kwanza baada ya michezo mitatu ya hatua hiyo ya makundi.

Robertinho amesema wamejipanga kuhakikisha wanashinda dhidi ya African Sports ili kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, ASFC.

Pia siku zote malengo ya Simba ni kushinda kila taji la michuano wanayoshiriki na kwa hali hiyo wanahitaji kupata ushindi katika mchezo wa leo.

Kocha huyo raia wa Brazil, alisema leo wanategemea kuwatumia wachezaji ambao hawapati nafasi kubwa kikosini kwa kuwa wiki ijayo wana mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers.

"Tumejipanga kuhakikisha tunashinda mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya African Sports, Simba ni timu kubwa na tunahitaji kushinda kila taji na tupo tayari.

"Tunategemea kuwatumia wachezaji ambao hawajapata nafasi kubwa kikosini kwa kuwa tuna mchezo wa marudiano nyumbani dhidi ya Vipers kwa hiyo tunaziangalia mechi zote,” alisema Robertinho.

Kwa upande wa Kocha wa African Sports, Mussa Rashid, alisema ana waheshimu Simba lakini wamejiandaa vizuri kuonyesha ushindani mkubwa katika mchezo huo.

"Tunatambua mchezo utakuwa na ushindani mkubwa na malengo yetu makubwa yalikuwa ni kufika na kucheza hatua ya 16-bora ya Kombe la Shirikisho," alisema kocha huyo.


Post a Comment

0 Comments