Ticker

6/recent/ticker-posts

Uongozi Yanga Watamba Kucheza Robo Fainali Kombe La Shirikisho Afrika

UONGOZI wa Yanga, umewahakikishia wanachama na mashabiki wake kwamba, wasiwe na wasiwasi wowote timu yao itacheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu.

Yanga ipo nafasi ya pili kwenye Kundi D la michuano hiyo inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa imekusanya pointi nne, baada ya kucheza mechi tatu, ikishinda moja, sare moja na kupoteza moja.

Akizungumza mara baada ya mchezo dhidi ya Real Bamako uliochezwa nchini Mali na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema kwa hesabu walizonazo kila kitu kinakwenda sawa.

“Mwananchi usiwe na mashaka kwa pointi moja ambayo tumepata ugenini, hii sio mbaya, ni mwanzo mzuri kwetu, tunakwenda kuweka historia mpya kwa kutinga hatua ya robo fainali.

“Tumedhamiria na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kazi kubwa na ngumu hasa kwa mechi zetu mbili Uwanja wa Mkapa, tunapambana kupata pointi sita ili kusonga mbele, hapo hesabu zitajibu.

“Ninaona wapo ambao wameanza kukata tamaa, hilo wasiwe nalo kabisa, Wananchi watembee kifua mbele, tunafanya kazi kubwa kufikia malengo yetu, lazima tushirikiane,” alisema Kamwe.

Mechi tatu zilizosalia za Kundi D, Yanga itacheza mbili nyumbani dhidi ya Real Bamako na US Monastir ambapo Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amedhamiria kuwashushia vipigo wapinzani wake hao.

Baada ya hapo, itakwenda DR Congo kumalizana na TP Mazembe katika mchezo wa mwisho wa kundi hilo, huku hesabu za Yanga ni kuona inashinda mechi mbili zijazo ili kufikisha pointi kumi wanazoamini zitawavusha kwenda robo fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Yanga yatabiriwa makubwa Kombe la Shirikisho Barani Afrika 2023

Post a Comment

0 Comments