Ticker

6/recent/ticker-posts

NMB kudhamini Mapinduzi Cup 2023, Simba na Yanga

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

BENKI ya NMB itakuwa mdhamini mashindano ya kombe la Mapindizi 2023 yanayotarajiwa kuanza Januari 1, 2023 katika Uwanja wa Amaan Unguja, Pemba kwa kutoa kiasi cha zaidi ya Sh33 milioni.


Kiasi hicho kitatumika kutoa zawadi ya fedha taslimu Sh23 milioni kwa mshindi wa jumla na kununua vifaa vya mazoezi yaani tracksuits kwaajili ya viongozi, mpango ambao unasaidia benki hiyo kutimiza ahadi yake ya kusaidia maendeleo ya michezo.


Mashindano ya Mapinduzi 2023 yanatarajiwa kuzinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi.


Katika mashindano hayo yatazikutanisha timu 12 ambapo timu tano zitatoka bara zikiwemo Yanga, Simba, Azam, Singida Big Stars na Namungo.


Timu nyingine tano zinatoka visiwani Zanzibar ni pamoja na KVZ, KMKM, Malindi, Mlandege, Jamhuri na Chipukizi huku timu moja ya Burundi ikiwa Aigle Noir Makamba FC.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza udhamini wa benki hiyo katika Ofisi za Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Meneja Mkuu wa Bishara wa Benki ya NMB Tawi la Zanzibar, Naima Said Shaame alisema udhamini unalenga azma ya benki hiyo na juhudi za Serikali katika kusherehekea miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.


“Tukiwa miongoni mwa wadau wakubwa wanaochangia ukuaji wa wa sekta mbalimbali za a maendeleo nchini Zanzibar, tuliona ni wajibu wetu kuwa sehemu ya maadhimisho haya. Tumekuwa tukiunga mkono michuano ya Mapinduzi tangu kuanzishwa kwake na tunaamini msaada wetu utasaidia kufanya mashindano ya mwaka huu kuwa makubwa na bora,” alisema.


Naima alisema mbali na kukabidhi zawadi kubwa ya milion 23 kwa mshindi wa masindano hayo, benki hiyo pia imetoa msaada wa vifaa vya mazoezi yaani ‘tracksuits’ kwa viongozi mbalimbali na wanadiplomasia ambao watashiriki katika matembezi yatakayofanyika Pemba kuashiria ufunguzi wa mashindano hayo.


“Huu sio mwisho wa udhamini wetu. Hivi karibuni tutatangaza mipango mingine ya ufadhili mara tu baada ya kufikia makubaliano na wizara inayohusika. Kama benki, tutaendelea kushirikiana na Serikali ili kuimarisha maendeleo ya michezo nchini kote. Benki ya NMB inaamini kwamba michezo sio tu inachangia ustawi wetu, lakini pia inatuleta pamoja kama taifa,” alisema Shaame.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab wakati wa hafla hiyo aliipongeza benki hiyo kwa msaada wake huku akisisitiza kuwa msaada huo umekuja kwa kwani wizara hiyo imekuwa ikipambana kutafuta wadhamini.


“Udhamini wa benki ya NMB sasa unatupa imani kuwa mashindano ya Mapinduzi yanoyotarajia kufunguliwa Januari Mosi mwakani sasa yatafanikiwa.


“Tayari tumeshapokea fedha taslimu kwa mshindi wa michuano hiyo na zawadi nyingine za mfungaji bora, Timu yenye nidhamu bora, Mfungaji Bora na hizi zitakabidhiwa mbele ya Rais wa Zanzibar,” alisema Shaame 


Alisisitiza dhamira ya wizara yake ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Zanzibar ili kuimarisha maendeleo ya michezo.


“Ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo ya michezo utahakikisha ukuaji wa michezo kwa muda mrefu. Nachukua fursa hii kuhimiza makampuni mengine kujitokeza na kuunga mkono juhudi za serikali za kukuza maendeleo ya michezo,” aliongeza.Post a Comment

0 Comments