Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uingereza Kuvaana Na Senegal Raundi Ya 16-Bora Baada Ya Kuiondosha Wales

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

MABAO MAWILI aliyofunga MARCUS Rashford yaliwezesha Uingereza kukamilisha kampeni zao za makundi kwenye Kombe la Dunia kileleni mwa Kundi B baada ya kutandika majirani zao Wales 3-0 uwanjani Ahmad Bin Ali.

Uingereza waliofungiwa bao jingine na Phil Foden, sasa watamenyana na Senegal katika hatua ya 16-bora mnamo Disemba 4, 2022 ugani Al Bayt.

Miamba hao wanaowinda ubingwa wa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1966, walikifanyia kikosi chao kilitoka sare tasa na Amerika mnamo Novemba 25 mabadiliko manne. Rashford, Foden, Jordan Henderson na Kyle Walker walijaza nafasi za Raheem Sterling, Bukayo Saka, Mason Mount na Kieran Trippier.

Uingereza walishuka dimbani wakihitaji ushindi au sare ili kutinga raundi ya muondoano. Kwa upande wao, Wales walikuwa na ulazima wa kuzoa alama tatu na kutarajia pambano jingine la Kundi B kati ya Amerika na Iran likamilike kwa sare. Hata hivyo, Amerika walikomoa Iran 1-0 uwanjani Al Thumama.

Matumaini ya Wales kusonga mbele kwenye fainali za Kombe la Dunia wanazozinogesha kwa mara ya kwanza tangu 1958, yalididimizwa na Iran baada ya kichapo cha 2-0 mnamo Novemba 25, 2022 ugani Ahmad Bin Ali.

Ushindi uliosajiliwa na Amerika dhidi ya  Iran ugani Al Thumama mnamo Jumanne usiku, uling’niniza Wales  pembamba zaidi kwa kuwa walijipata katika ulazima wa kufunga Uingereza angalau mabao manne kwa nunge ili kusonga mbele.

Chini ya kocha Robert Page, Wales sasa hawajashinda mechi yoyote kati ya nane zilizopita katika mashindano yote. Hii ni mara yao ya kwanza kumaliza kampeni za mashindano ya haiba kubwa bila kusajili ushindi.

Alama tatu zilizovunwa na Uingereza ziliwapa uhakika wa kudhibiti kilele cha Kundi B na hivyo kukutana na kikosi Senegal waliokomoa Ecuador 2-1 na kuambulia nafasi ya pili kwenye Kundi A lililoshuhudia Uholanzi wakitandika Qatar 2-0 katika mechi yao ya tatu na ya mwisho katika hatua ya makundi.

Japo Uingereza na Wales waliwahi kukutana mara 103 awali katika historia, pambano la Jumanne usiku lilikuwa lao la kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia. Chini ya kocha Gareth Southgate, Uingereza sasa wameshinda michuano saba mfululizo iliyopita dhidi ya Wales.

Wales waliofungua kampeni za Kundi B kwa sare ya 1-1 dhidi ya Amerika, walikosa maarifa ya golikipa wao tegemeo, Wayne Hennessey, aliyeonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Iran katika pambano la awali.

Post a Comment

0 Comments