Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Uholanzi Waifunga Qatar Katika Kundi A Na Kuingia Hatua Ya 16-Bora

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

MSHAMBULIAJI Cody Gakpo alifunga bao na kusaidia Uholanzi kuibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi ya wenyeji Qatar  katika mechi ya Kundi A iliyowakatia tiketi ya kuingia raundi ya 16-bora kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu.

Huku Uholanzi wakikamilisha kampeni zao za makundi kileleni mwa Kundi A kwa alama saba, Qatar waliokuwa tayari wameaga Kombe la Dunia, walipoteza mchuano wao wa tatu mfululizo.

Chini ya kocha Louis van Gaal, Uholanzi waliokosa kunogesha Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, wamefuzu kwa hatua ya 16-bora mwaka huu bila kupoteza mechi yoyote. Sasa watakutana na kikosi kitakachoambulia nafasi ya pili katika Kundi B linalojumuisha Uingereza, Amerika, Wales na Iran.

Mabingwa wa Afrika, Senegal walipepeta Ecuador katika pambano jingine la Kundi A na kumaliza kampeni zao katika nafasi ya pili. Ilivyo, masogora hao wa kocha Aliou Cisse sasa watakutana na Uingereza huku Uholanzi wakimenyana na Amerika katika raundi ya muondoano.

Gakpo ambaye ni fowadi matata wa PSV Eindhoven sasa amefunga bao la kwanza katika mechi zote tatu ambazo zimesakatwa na Uholanzi katika hatua ya makundi.

Bao la pili la Uholanzi lilijazwa wavuni na Frenkie de Jong aliyeshirikiana vilivyo na Memphis Depay, Davy Klaassen, Virgil van Dijk na Gakpo anayehusishwa pakubwa na Manchester United.

Gakpo, 23, sasa ndiye mchezaji wa kwanza wa Uholanzi kuwahi kufunga bao katika mechi zake tatu za kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia. Nyota huyo sasa amehusika katika mabao 35 kutokana na mechi 29 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa ambapo amefunga magoli  17 na kuchangia mengine 18.

Mbali na kupigwa katika mechi tatu mfululizo kwenye makala yao ya kwanza katika Kombe la Dunia, Qatar pia walifungwa mabao saba, idadi hiyo ikiwa ya juu zaidi kwa taifa ambalo ni mwenyeji wa kipute hicho kuwahi kupokezwa katika hatua ya makundi.

Huku makala ya 23 ya Kombe la Dunia 2026 yakishirikisha timu 48 badala ya 32, Qatar wana fursa nyingine ya kufuzu kwa kipute hicho, mara hii kwa kupitia mchujo baada ya uenyeji kuwapa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki fainali za mwaka huu.

Uholanzi walishuka dimbani dhidi ya Qatar ugani Al Bayt wakijua ushindi au sare ya aina yoyote ingewawezesha kuingia raundi ya muondoano. Wanafainali hao wa Kombe la Dunia 2010 bado wangefuzu kwa hatua ya 16-bora iwapo watalazwa na Qatar nao Ecuador wazamishe chombo cha Senegal.

Kufikia sasa, Uholanzi wanajivunia alama saba, moja kuliko Senegal. Ecuador ni wa tatu kundini kwa alama nne huku Qatar wakivuta mkia bila pointi yoyote.

Ecuador wangetinga hatua ya 16-bora wakiwa kileleni mwa Kundi A iwapo wangenyuka Senegal mabao mengi kuliko idadi ya magoli ambayo Uholanzi iliwafunga Qatar. Zawadi ya kumaliza kileleni ni kukutana na Amerika –  nambari pili katika Kundi B linalojumuisha pia Iran, Wales na Uingereza watakaovaana na Senegal.

Licha ya kutoshana nguvu na Ecuador kwa sare ya 1-1 katika mchuano wao wa pili katika Kundi A, Uholanzi wanajivunia ufufuo mkubwa wa makali yao chini ya kocha Van Gaal aliyewaongoza kufuzu kwa fainali za makala ya tatu ya UEFA Nations League mwaka huu wa 2022.

Uholanzi walikosa Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi baada ya kutinga nusu-fainali za 2014 nchini Brazil wakinolewa na Van Gaal. Miamba hao ni miongoni mwa timu kubwa katika ulingo wa soka ambazo hazijawahi kunyanyua Kombe la Dunia.

Walipoteza fainali ya 1974, 1978 na 2010 dhidi ya Ujerumani (2-1), Argentina (3-1) na Uhispania (1-0) mtawalia. Argentina iliwabandua kwa penalti 4-2 kwenye nusu-fainali za 2014 baada ya sare tasa.

Post a Comment

0 Comments