Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Senegal Waifunga Ecuador Katika Kundi A Na Kujikatia Tiketi Ya 16-Bora

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

BEKI Kalidou Koulibaly alifungia Senegal bao la pili katika ushindi wa 2-1  dhidi ya Ecuador katika mchezo wa mwisho wa Kundi A katika uwanja wa Khalifa International.

Matokeo hayo yaliwezesha Senegal kutinga hatua ya 16-bora ya fainali za Kombe la kwa mara ya pili katika historia.

Mabao yote matatu katika mechi hiyo yalifumwa kimiani na wanasoka wa ligi za Uingereza. Moises Caicedo wa Brighton alifungia Ecuador bao lililofuta juhudi za IsmaiL Sarr aliyeweka Senegal kifua mbele kabla ya Koulibaly wa Chelsea kuwafungia bao la ushindi.

Ecuador walishuka dimbani wakihitaji alama moja pekee ili kuingia raundi ya muondoano. Penalti iliyofungwa na Sarr ilitokana na tukio la kuangushwa kwake na Piero Hincapie ndani ya kijisanduku mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Ecuador alisawazisha mambo katika dakika ya 67 baada ya kumegewa krosi safi na Felix Torres. Senegal sasa watakutana na kikosi kitakachotamalaki Kundi B linalojumuisha Uingereza, Amerika, Wales na Iran.

Senegal waliwahi kuingia robo-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002 baada ya kuduwaza waliokuwa mabingwa watetezi Ufaransa katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi A. Hata hivyo, kikosi hicho kilichotambishwa zaidi na El Hadji Diouf na aliyekuwa kiungo wa Fulham na Portsmouth,  Papa Bouba Diop, kilidenduliwa na Uturuki katika raundi ya nane-bora. Dioup aliaga dunia mnamo 2020 akiwa na umri wa miaka 42.

Mbali na kutokuwepo kwa fowadi tegemeo Sadio Mane anayeuguza jeraha la mguu, pigo zaidi kwa Senegal katika pambano lao la hatua ya 16-bora mwaka huu ni kukosekana kwa kiungo Idrissa Gueye Gana ambaye ameonyeshwa kadi mbili za manjano kwenye fainali za mwaka huu. Mechi hiyo ya hatua ya muondoano ingekuwa ya 100 kwa kiungo huyo ndani ya jezi za Senegal.

Senegal waliokomoa Misri mnamo Februari 2022 na kujizolea Kombe la Afrika (AFCON), walianza kampeni za Kundi A kwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Uholanzi kabla ya kupepeta wenyeji Qatar 3-1 katika mchuano wa pili. Ecuador walitandika Qatar 2-0 katika mechi ya kwanza kabla ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Uholanzi.

Ecuador wangetinga hatua ya 16-bora wakiwa kileleni mwa Kundi A iwapo wangenyuka Senegal mabao mengi kuliko idadi ya magoli ambayo Uholanzi ilifunga Qatar. Uholanzi walipepeta Qatar 2-0 katika mchuano wao wa mwisho ugani Al Bayt.

Kutokuwepo kwa fowadi Sadio Mane kambini mwa Senegal kuliacha kocha Aliou Cisse katika ulazima wa kutegemea tena maarifa ya Sarr na Famara Diedhiou walioshirikiana vilivyo na Iliman Ndiaye, Bamba Dieng na Krepin Diatta katika safu ya mbele.

Post a Comment

0 Comments