Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ujerumani Yalenga Mwanzo Bora Mwaka Huu Kwa Ushindi Dhidi Ya Japan Katika Kundi E

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

UJERUMANI watashuka ugani Khalifa International mnamo Novemba 23, 2022 wakilenga ushindi muhimu dhidi ya Japan katika Kundi E ili kuepuka makosa ya 2018 nchini Urusi.

Ujerumani almaarufu Die Mannschaft walidunguliwa mapema kwenye fainali za Kombe la Dunia katika hatua ya makundi miaka minne iliyopita huku Japan wakitinga raundi ya 16-bora ambapo waling’olewa na Ubelgiji.

Wakiwa chini ya kocha Joachim Loew wakati huo, Ujerumani walishindwa kutetea kwa mafanikio ubingwa wa Kombe la Dunia walioutwaa mnamo 2014 nchini Brazil baada ya kupepeta Argentina 1-0.

Badala yake, walifungua kampeni za Kundi F kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Mexico. Japo walitandika Uswidi 2-1 katika mchuano wa pili, walinyolewa kwa 2-0 na Korea Kusini katika pambano la tatu.

Ujerumani ambao ni mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia, waling’olewa na Uingereza kwenye hatua ya 16-bora ya fainali zilizopita za Euro 2020 kwa kichapo cha 2-0 ugani Wembley.

Matokeo hayo yalitamatisha kipindi cha ukufunzi wa Loew aliyejiuzulu na nafasi yake kutwaliwa na Hansi Flick aliyeagana na klabu ya Bayern Munich.

Japo wanapigiwa upatu wa kutwaa Kombe la Dunia mwaka huu, Ujerumani wana rekodi duni ya kushinda mechi mbili pekee kutokana na nane zilizopita. Aidha, waliambulia nafasi ya tatu kwenye kundi lao la UEFA Nations League lililojumuisha pia Italia na Uingereza. Hata hivyo, watajibwaga ulingoni dhidi ya Japan wakijivunia kushinda Oman 1-0 katika pambano lao lililopita la kirafiki.

Ushindi dhidi ya Japan utawapa motisha zaidi ya kunyoa Costa Roca na Uhispania ambao ni washindani wao wengine katika Kundi E. Ujerumani wanaolenga kufikia rekodi ya Brazil ambao ni washindi mara tano wa Kombe la Dunia, ndicho kikosi cha pili baada ya wenyeji Qatar kufuzu kwa fainali za mwaka huu.

Mechi dhidi ya Mexico mnamo 2018 nchini Urusi ilikuwa ya kwanza tangu 1986 kwa Ujerumani kupoteza katika pambano lao la ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia.

Hadi mwaka wa 2018, Japan walikuwa wamezoea kuondolewa katika hatua ya makundi kwenye makala matano mfululizo ya fainali za Kombe la Dunia kuanzia 1998.

Hata hivyo, wanajivunia rekodi nzuri ya kushinda mechi 15 kati ya 18 zilizopita huku wakifunga jumla ya mabao 58. Japan wameshinda michuano mitano pekee kutokana na 21 iliyopita kwenye fainali za Kombe la Dunia. Walifungua kampeni zao za makundi mnamo 2018 kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Colombia.

Ujerumani waliwahi kukutana na Japan mnamo 2004 kirafiki na wakasajili ushindi wa 3-0 kabla ya kuambulia sare ya 2-2 miaka miwili baadaye.

Pigo kubwa kwa Ujerumani ni kukosekana kwa kiungo mkabaji Marco Reus ambaye pia alikosa fainali za Euro 2016, Euro 2020 na Kombe la Dunia 2014 kutokana na majeraha. Hata hivyo, miamba hao wanajivunia marejeo ya vigogo Niclas Fullkrug, Thomas Muller na Antonio Rudiger ambao wamepona majeraha.

Muller aliyewahi kutemwa kabisa katika timu ya taifa kabla ya kurejeshwa, amefunga mabao 10 na kuchangia sita mengine kutokana na mechi 16 za Kombe la Dunia.

Japan watategemea zaidi maarifa ya kiungo Hidemasa Morita wa Sporting Lisbon, beki Takehiro Tomiyasu wa Arsenal, fowadi Takuma Asano na nahodha Maya Yoshida ambaye amewajibikia timu yake ya taifa mara 122.

Post a Comment

0 Comments