Ticker

6/recent/ticker-posts

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ujerumani Na Uhispania zatoshana Nguvu

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Mshambuliaji NICLAS Fuellkrug alifunga bao lililozolea Ujerumani alama muhimu katika mechi ya Kundi E iliyokamilika kwa sare ya 1-1 kati yao na Uhispania mnamo Jumapili usiku katika dimba la  Al Bayt.

Matokeo ya pambano hilo liliweka hai matumaini ya Ujerumani kufuzu kwa hatua ya muondoano kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu. Kichapo kwa Ujerumani waliofungua kampeni zao nchini Qatar kwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Japan, kingetosha kuwadengua mapema kwenye hatua ya makundi.

Chini ya kocha Hansi Flick, Ujerumani sasa wana ulazima wa kuangusha Costa Rica katika pambano lao la mwisho la Kundi E kwa matarajio kwamba Japan hawatatamalaki pambano litakalowakutanisha na Uhispania.

Uhispania walijiweka kifua mbele katika dakika ya 62 kupitia kwa Alvaro Morata aliyetokea benchi katika kipindi cha pili na kujaza kimiani krosi ya Jordi Alba.

Hata hivyo, Ujerumani walisawazisha mambo kupitia kwa Fullkrug aliyemwacha hoi kipa Unai Simon dakika saba kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa. Leroy Sane alipoteza nafasi murua ya kufungia Ujerumani bao la ushindi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Kocha Luis Enrique ambaye amesuka kikosi chenye mseto wa wanasoka wazoefu na chipukizi, analenga kuongoza Uhispania kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2010 walipotawazwa wafalme nchini Afrika Kusini.

Mbali na chipukizi Gavi, 18, na Pedri, 20, Uhispania wanajivunia pia maarifa ya masogora wenye tajriba pevu kama vile Sergio Busquets, Dani Alba, Aymeric Laporte na Rodri.

Gavi ambaye huchezea Barcelona, alifunga bao katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Costa Rica mnamo Novemba 23, 2022 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa umri mdogo zaidi kuwahi kufunga bao katika historia ya Kombe la Dunia baada ya Pele mnamo 1958.

Ujerumani sasa wana ulazima wa kutandika Costa Rica mnamo Alhamisi ili kufuzu kwa raundi ya 16-bora iwapo Japan watashindwa kulaza Uhispania.

Post a Comment

0 Comments