Ticker

6/recent/ticker-posts

Kombe la Dunia: Saka wa Arsenal Aiongoza Uingereza kuitandika Iran 6-2 nchini Qatar

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Timu ya taifa ya Iran imeanza vibaya kampeni yake katika Kombe la Dunia la mwaka 2022 nchini Qatar kwa kupokea kichapo kikubwa cha 6-2 kutoka kwa timu ya taifa ya Uingereza - Three Lions. 

Bukayo Saka, Jude Bellingham, Raheem Sterling, Marcus Rashford na Jack Grealish wote walitikisa nyavu kwa faida ya Uingereza huku Mehdi Taremi akifunga mabao ya Iran. 

Kipindi cha kwanza Iran walikutwa na majanga katika dakika ya 16 baada ya kipa wao Alireza Beiranvand alipongana na mchezaji wake Majid Hosseini. 

Licha ya kufanyiwa gangaganga kwa dakika kadhaa, Beiranvand alishindwa kuendelea na mchezo akiondolewa uwanjani kwa machela na nafasi yake kuchukuliwa na Hosseini Hosseini. 

Bellingham ambaye hupiga soka yake na Borussia Dortmund ya Ujerumani alivunja ubikra wa Iran katika dakika ya 35 kwa bao la kichwa. 

Saka ambaye amekuwa mchezaji wa kutegemewa katika klabu ya Arsenal alifunga bao la pili la Uingereza katika dakika ya 43 kabla ya Sterling kufanya mambo kuwa 3-0 katika dakika za ziada za kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili Saka alifunga bao lake la pili katika dakika ya 62 kabla ya Taremi kusukuma kombora lilimpita kipa Jordan Pickford na kuwapa goli Iran dakika tatu baadaye. 

Rashford alifanya mambo kuwa 5-1 kwa faida ya Uingereza katika dakika 71 - sekunde chache tu baada ya kuingizwa mchezoni - huku Grealish akipiga msumari mwa mwisho katika dakika ya 90. 

Iran walipata penalti katika dakika ya 13 ya nyongeza, Taremi akifunga bao lake la pili na mchezo huo wa kundi B kukamilika 6-2. 

Post a Comment

0 Comments