Ticker

6/recent/ticker-posts

Vita ya namba Yatikisa Simba, Mastaa wajifua ili kupata namba kikosi cha kwanza

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

SIMBA jana usiku ilishuka dimbani kucheza mechi yake ya mwisho ya mashindano maalumu huko Sudan dhidi ya wenyeji, Al Hilal, Lakini Kocha Mkuu wa Simba, Zoran Maki, bado amekuwa na maingizo tofauti katika kikosi chake cha kwanza cha Wekundu hao wa Msimbazi.

Wakati Akihojiwa hapo jana, Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, alisema wachezaji wa timu hiyo wamekuwa na ushindani mazoezini na katika mechi zote walizocheza kwa sababu hakuna ambaye anaamini amepata namba ya kudumu.

Matola alisema kupata michezo mingi ya kirafiki pia kumesaidia kuwaimarisha wachezaji wao kwa sababu wanakabiliwa na mechi ngumu za Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanayokwenda kushiriki.

"Bado tunasuka kikosi, tumekuwa tukiwatumia wachezaji tuliokuwa nao hapa katika michezo hii kwa maana ya kuwaimarisha zaidi, ninaamini baada ya mashindano haya mwalimu (Maki), atakuwa amepata kikosi chake," alisema Matola.

Aliongeza kuna wachezaji ambao msimu uliopita walionekana wamejihakikishia namba lakini kwa sasa hali imebadilika, hivyo mabadiliko haya yanawafanya nyota wetu kuendelea kujituma zaidi.

"Mechi hizi zimetusaidia kuelekea mechi yetu ya kimataifa dhidi ya Big Bullet ya Malawi, zimetupa nafasi ya kuwaangalia wachezaji ambao hawakupata nafasi, tumewaangalia wachezaji wengine ambao hawakupata nafasi na kupata picha halisi ya timu nzima," Matola alisema.

Aliongeza wakati wanaendelea na michezo hiyo, benchi la ufundi limeendelea kuwafuatilia wapinzani wao, Big Bullet ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuvuna matokeo chanya.

"Siku hizi hakuna timu ndogo, tutaenda Malawi kuwakabili wapinzani wetu kwa tahadhari zote, hatutaki kuwa na mlima mkubwa tutawapowaalika katika mechi ya marudiano nyumbani, tumejipanga kufika mbali," Matola alisema.

Wakati huo huo, kiungo, Sadio Kanoute, raia wa Mali na nahodha, John Bocco walijiunga na timu hiyo iliyoko Sudan tangu juzi na kukiongezea nguvu kikosi chao.

"Ujio wa Kanoute na Bocco ni faraja kwetu, kunaendelea kumpa wigo kocha na hatimaye baada ya kumaliza mechi hizi, tutakuwa na mwanga wa wapi tutakwenda," aliongeza kocha na nahodha huyo wa zamani wa Simba.

Katika hatua nyingine, Kanoute, Pape Sakho na Clatous Chama wametajwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Agosti wa Simba.

Hata hivyo, rekodi zinampa nafasi kubwa ya Chama ambaye amecheza mechi mbili za ligi na kufunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar kushinda tuzo hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Emirate Aluminium.


Post a Comment

0 Comments