Ticker

6/recent/ticker-posts

TFF wazuia Usajili wa Tuisila Kisinda Yanga

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

TAARIFA ya kushtua kwa mashabiki wa Yanga ni usajili wa winga wao, Tuisila Kisinda umekumbana na sintofahamu kubwa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya klabu hiyo kuandikiwa barua wakizuiwa kuwa naye, jambo lililowafanya mabosi hao kushangazwa na amri hiyo.

Yanga ilimsajili Kisinda kwa mkopo akitokea RS Berkane ya Morocco iliyowauziwa msimu uliopita mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021. Hata hivyo, wakati mashabiki wakianza kuhesabu saa za kumshuhudia winga huyo akiungana na wachezaji wenzake, taarifa za kuaminika ni kwamba, TFF imeiandika barua Yanga kuwazuia kumleta Kisinda nchini kwa madai haiwezi kumtumia kwenye Ligi Kuu inayorejea kesho.

Barua hiyo imesainiwa na mmoja wa viongozi wa juu wa TFF, japo inafahamika Yanga ilifanya kila kitu kwa wakati kumsajili Kisinda kabla ya dirisha la usajili kufungwa saa 5.59 usiku wa Agosti 31 iliyokuwa siku ya mwisho ya usajili wa wachezaji nchini.

Mbali na kuwahi usajili wa Kisinda kwa wakati, lakini pia Berkane ilituma hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC) ndani ya muda.

Hata hivyo Yanga imezuiwa kupitisha usajili wa winga huyo Mkongomani kwa madai tayari walishakuwa na mchezaji mwingine waliyemwombea uhamisho. Hesabu za Yanga ni katika kumsajili Kisinda walimwondoa mshambuliaji Lazarous Kambole kutoka Zambia katika hesabu zao kabla ya dirisha kufungwa kutokana na Mzambia huyo kuwa katika majeruhi makubwa ya muda mrefu na kushindwa kuitumikia timu hiyo.

“Wakati tunamsajili Kisinda tulishajipanga tumwondoe nani na huku kwetu tulishamwondoa Kambole (Lazarous) kwa kuwa tuliona hali yake ya majeruhi itatupa shida, tumemwondoa katika mfumo ili nafasi yake ichukuliwe na Kisinda,” alisema bosi mmoja wa Yanga (jina tunalo) na kuongeza;

“Ghafla jana tukapokea barua kutoka TFF kutoka kwa (anamtaja bosi huyo mkubwa wa TFF) akisema hawatapitisha usajili wa Kisinda kwa maelezo eti tulishaanza kumwombea uhamisho mchezaji mwingine.

“Tunajiuliza mbona zipo klabu nyingi tu hapa ziliwaleta wachezaji wao na wamewaondoa katika usajili wa msimu ujao bila kufanyiwa ambacho sisi Yanga tumefanyiwa.”

Kabla ya ujio wa Kisinda Yanga tayari walishakuwa na wachezaji 12 kama hitaji ya kikanuni ambao ni kipa Diarra Djigui, mabeki Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yannick Bangala, viungo Khalid Aucho Gaely Bigirimana, mawinga Bernard Morrison, Jesus Moloko na washambuliaji Heritier Makambo, Kambole na Fiston Mayele.

Katika ujio wa Kisinda, Yanga iliamua kumwondoa Kambole ambaye tangu amefika ameshindwa kucheza hata mchezo wa kirafiki kutokana na majeruhi akiungana na Yacouba Songne aliyeachwa kikosini licha ya kutotumika kwenye mechi za ligi na wala hakutambulishwa na klabu hiyo.

Yanga sasa imepanga kulalamika kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wakigomea uamuzi huo huku wakiona kuna hujuma zinasukwa kupunguza makali ya timu yao.

“Kuna mkono wa mtu katika hili na Yanga tunasema hatutakubali, tutapinga kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji, lakini tunaona hapa kuna hila zinataka kufanyika kutupunguza nguvu kwa kuwa wapo ambao wamekuwa wakipambana hata kumzuia mchezaji asije kujiunga na Yanga wakakwama, inawezekana sasa wamehamia kwingine kupambana na mpango huo,” alisema kigogo huyo wa Yanga.

Hakuna kiongozi wa TFF aliyepatikana jana kufafanua juu ya taarifa barua hiyo ya zuia la Kisinda kuitumikia Yanga.

Post a Comment

0 Comments