Ticker

6/recent/ticker-posts

Okwa: Sasa nipo tayari kwa kazi

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

BAADA ya kukiona kikosi cha Simba kinavyoendelea kujifua, kiungo mshambuliaji, Mnigeria Nelson Okwa ameweka wazi kwamba yuko tayari kwa kazi na anayatamani zaidi mashindano ya kimataifa anayoamini watatisha huko kutokana na maandalizi waliyoyafanya.

Okwa aliyesajiliwa na Simba kutoka Rivers United ya kwao Nigeria katika dirisha hili la usajili amefunguka hayo kwa njia ya simu kutokea Sudan anakoendelea kujifua na Simba.

Okwa ameliambia Mwanaspoti kuwa yuko vizuri kwa sasa na mechi hizo zinawaweka sawa kisaikolijia kushindana kimataifa zaidi kwani ni aina ya timu ambazo watakutana huko hivyo yanawakomaza.

“Tunakutana na timu ambazo zinashiriki mashindano ya CAF pamoja na kuwa ni sehemu ya maandalizi kwetu lakini yanatujenga kiakili kuhakikisha tunakuwa imara na wazoefu tutakapokutana na wapinzani wetu,” alisema na kuongeza;

“Asante Kotoko na Al Hilal ni wapinzani wetu kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa kujipima nao inatupa ari ya kujiamini zaidi siku tutakapokutana nao kwenye mechi za mashindano ata tusipokutana nao bado sisi kama wachezaji tutakuwa tumejengeka kiakili,” alisema mchezaji huyo ambaye alichelewa kujiunga na Simba msimu huu wa mashindano.

Akizungumzia ugumu wa Ligi za Tanzania alifafanua kwa kubainisha kuwa katika michezo miwili aliyocheza pamoja na kuanzia benchi amegundua kuwa anacheza ligi ambayo inahitaji kasi na nguvu.

“Nilichukulia kawaida kuingizwa kipindi cha pili mimi kama mchezaji iliniongezea kitu kwani nilipata nafasi ya kuwasoma wapinzani wangu na mara baada ya kuingia nilitumia mapungufu niliyoyaona na kuisaidia timu kuibuka na ushindi,” alisema mchezaji huyo.

“Kama timu itaendelea na matokeo mazuri kwenye mechi zinazofuata sioni timu ya kuizuia kutokana na timu kuendelea kuboreshwa zaidi na benchi la ufundi na wachezaji wenyewe kwa kuhitaji nafasi ya kucheza mara kwa mara.”

Okwa alisema timu yoyote inayopata matokeo inaongeza ari na kutokana na wingi wa wachezaji wageni ndani ya timu kunatoa nafasi ya kocha kuendelea kutengeneza timu huku wachezaji nao wakitumia nafasi hiyo kujitengenezea mazingira ya kuwa bora kwa kujihakikishia nafasi ya kucheza.

Post a Comment

0 Comments