Ticker

6/recent/ticker-posts

Nyota Watatu wa Arsenal Watemwa Kikosi Cha Timu ya Taifa ya Brazil

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KOCHA  Mikel Arteta amechangamkia maamuzi ya kocha Adenor Tite Bacchi wa Brazil kutowaita kambini wachezaji watatu tegemeo wa Arsenal katika kikosi anachokiandaa kwa mechi zijazo za kirafiki.

Beki Gabriel Magalhaes, mvamizi Gabriel Jesus na fowadi Gabriel Martinelli wameachwa nje ya timu ya Brazil itakayopimana nguvu na Ghana na Tunisia mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba.

Hata hivyo, mabingwa hao mara tano wa dunia watawajibisha masogora 11 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika michuano hiyo itakayokuwa sehemu ya maandalizi ya fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Alisson Becker (Liverpool), Ederson Moraes (Man-City), Thiago Silva (Chelsea), Bruno Guimaraes (Newcastle), Lucas Paqueta (West Ham United) na Carlos Casemiro (Man-United) ni miongoni mwa wachezaji wa EPL watakaounga kikosi cha Brazil.

Wengine ni Fabinho Tavares (Liverpool), Fred Rodrigues (Man-United), Antony dos Santos (Man-United), Roberto Firmino (Liverpool) na Richarlison Andrade (Tottenham).

Licha ya wachezaji watatu mahiri wa Arsenal kutemwa, Arteta anahisi kuwa maamuzi hayo ya Tite yataepushia kikosi chake visa vya majeraha na hivyo kuwapa uhakika wa kuendelea kujivunia uthabiti ambao kwa sasa unawadumisha kileleni mwa jedwali la EPL.

Baada ya kushinda mechi tano kati ya sita za kwanza katika EPL msimu huu, Arsenal wanajivunia alama 15, moja zaidi kuliko Spurs na mabingwa watetezi Man-City wanaopigania taji la tatu mfululizo ligini, la saba katika historia na la tano chini ya kocha Pep Guardiola aliyeanza kudhibiti mikoba yao mnamo 2016-17.

“Wanasoka wetu wataepuka hatari ya kupata majeraha mabaya kutokana na mechi za kirafiki. Ni nafuu zaidi kwamba hakuna yeyote ataitwa kuwa sehemu ya kikosi cha Brazil. Itakuwa fursa nzuri kwao kupumzika na kujifua zaidi kwa kibarua kigumu kilichoko mbele,” akasema Arteta.

Arsenal watashuka dimbani Alhamisi wiki ijayo kuvaana na PSV Eindhoven ya Uholanzi katika pambano la Europa League ugani Emirates baada ya gozi la EPL lililokuwa liwakutanishe na Everton wikendi hii kuwa sehemu ya mechi zilizoahirishwa kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II. Kikosi hicho kitamenyana baadaye na Brentford, Spurs, Bodo/Glimt na Liverpool kwa usanjari huo.

Huku Tunisia na Ghana wakivaana na Brazil, Cameroon wamepangiwa mechi mbili za kirafiki nchini Korea Kusini. Watavaana na Uzbekistan mnamo Septemba 23 kabla ya kushuka dimbani kupimana nguvu na Korea Kusini siku nne baadaye jijini Seoul.

Senegal almaarufu Teranga Lions, watamenyana na Bolivia mnamo Septemba 24 nchini Austria kabla ya kuvaana na Iran. Ghana, Tunisia na Morocco ni mataifa mengine yatakayowakilisha bara la Afrika kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar. Morocco watapimana nguvu na Chile pamoja na Paraguay nchini Uhispania mnamo Septemba 23 na 27 mtawalia.

Cameroon wametiwa katika Kundi G pamoja na Brazil, Serbia na Uswisi. Senegal ambao ni wafalme wa Afrika, wamepangwa katika Kundi A kwa pamoja na Ecuador, Uholanzi na wenyeji Qatar.

Ghana ambao pia watachuana na Uswisi kirafiki mnamo Novemba, wametiwa katika Kundi H ambalo pia linajumuisha Ureno, Korea Kusini na Uruguay.

Tunisia wako katika Kundi D kwa pamoja na Australia, Denmark na mabingwa watetezi, Ufaransa. Morocco kwa upande wao watachuana na Ubelgiji, Canada na Croatia katika Kundi F.

Michuano ya Kombe la Dunia imeratibiwa kuanza Novemba 20 kwa pambano kati ya Ecuador na wenyeji Qatar. Fainali itatandazwa Disemba 18.

Vikosi 32 vitakavyonogesha fainali hizo nchini Qatar vina wiki moja pekee kujiandaa huku wachezaji wakitarajiwa kujiunga na timu zao za taifa kuanzia Novemba 13, 2022.

Post a Comment

0 Comments