Ticker

6/recent/ticker-posts

Moallin: Nilitamani kuendelea, naheshimu maamuzi

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin amesema kwamba anaheshimu maamuzi ya uongozi wa timu hiyo baada ya kuondolewa kwenye majukumu hayo.

Akihojiwa jijini Dar es Salaam, Moallin alisema hakushangazwa na kilichotokea kwake kwa sababu hizo ni moja ya changamoto za siku zote kwenye kazi hiyo hivyo ataendelea kutoa ushirikiano wake kwa manufaa makubwa ya timu.

“Haikuwa muda sahihi kwangu kwa sababu nilitaka kuendelea na majukumu haya, klabu imefanya kile ambacho inaona ni bora hivyo naheshimu hilo kwani nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunapiga hatua kwa pamoja,” alisema Moallin.

“Ni muda wangu wa kupumzika, kufurahi nikiwa na familia kwa kipindi cha muda mchache na kusaidia pale ambapo wao wameona pananifaa.”

Moallin aliteuliwa kuchukua nafasi hiyo Januari 25 mwaka huu baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wakati akiwa na timu za vijana akichukua mikoba ya mtangulizi wake Mzambia, George Lwandamina aliyeondoka Desemba 13, 2021 kufuatia matokeo yasiyoridhisha.

Taarifa iliyotolewa juzi na klabu hiyo ilieleza licha ya Moallin kuondoshwa ila ataendelea kubaki kwenye benchi la ufundi huku timu hiyo kwa sasa ikiwa chini ya Mhispania, Dani Cadena aliyeletwa kikosini hapo kwa ajili ya kuwanoa makipa.

Cadena ni kocha wa zamani wa makipa wa klabu za Ligi Kuu Hispania (La Liga) Sevilla na Real Betis ambaye pia ameshafanya kazi nchini China na Asaudi Arabia huku akiwa na uzoefu mkubwa na elimu ya juu ya Shirikisho la Soka Barani Ulaya UEFA.

Post a Comment

0 Comments