Ticker

6/recent/ticker-posts

Bernard Morrison na Fiston Mayele warejea Mazoezini

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


KLABU ya Yanga juzi ilirudi mazoezini baada ya kuwapa wachezaji wake mapumziko ya siku tatu, habari nzuri kwa wanayanga ni kurejea kwa mastaa wawili Bernard Morrison ‘BM33’ na Fiston Mayele walioibua hofu kwa mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kuwa majeruhi.

Morrison alikosekana katika mechi mbili za kimataifa ambazo Yanga ilicheza dhidi ya Zalan FC na kuifunga nje ndani kwa jumla ya mabao 9-0 sambamba na ile ya Ligi Kuu Bara waliyoipasua Mtibwa Sugar 3-0, Huku straika Fiston Mayele akitoka uwanjani akichechemea baada ya kutupia hat-trick ya pili akiwazamisha mabingwa hao wa Sudan Kusini.

Yanga juzi ilirudi kazini ikianzia gym ambapo ilijifua kwa saa mbili chini ya kocha msaidizi, Cedric Kaze ambaye naye alishiriki kwa kukimbia sawa na wachezaji kwa baadhi ya mazoezi na kocha wa viungo Helmy Gueldich, raia wa Tunisia.

Mazoezi hayo yaliendelea ufukweni jana asubuhi  ambapo mastaa hao walitumia tena saa mbili pale Coco wakipiga kazi nzito kwa mazoezi tofauti ya kujenga pumzi na stamina ya mwili, huku Mayele na Morrison wakiliamsha sambamba na wenzao mwanzo mwisho.

Kitu kilichowavutia mashabiki wa timu hiyo ambao waliangalia mazoezi hayo ni kurejea kwa Mayele ambaye aliwashtua baada ya kupata maumivu katika mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na Mayele pia Morrison naye alikuwa sambamba na wenzake baada ya kukosa mechi tatu baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mchezo wa sare ya mabao 2-2 wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam.

Yanga ilikuwa na wachezaji 17 katika mazoezi hayo wakiwemo Yannick Bangala, Mayele, Joyce Lomalisa, Zawadi Mauya, Gael Bigirimana, Yusuf Athuman, Salum Abubakar ‘Sure boy, Morrison na Djuma Shaban, Heritier Makambo, Tuisila Kisinda, Bakari Mwamnyeto na Eric Johola.

Wengine ni; Dickson Ambundo, Jesus Moloko, Farid Mussa na Ibrahim Bacca, kwani wenzao akiwamo Stephane Aziz KI, Diarra Djigui, Abuutwalib Mshery, Dickson Job, David Bryson, Denis Nkane na Shomary Kibwana wako na timu za taifa za Tanzania, Mali na Burkina Faso.

Baada ya mazoezi hayo Helmy alisema: “Tulikuwa na mapumziko ya siku mbili tatu hivi ni lazima tuwe na mazoezi kama haya tunaporejea, lakini hii ni kuweka miili sawa kuelekea mechi zinazokuja, ratiba inayokuja ni ngumu lazima tuongeze utayari wa miili.”


Post a Comment

0 Comments