Ticker

6/recent/ticker-posts

Yanga, Azam FC watambiana kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Septemba 6

MABOSI wa Yanga na Azam FC wametamba kila kikosi kiko tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Septemba 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Yanga itashuka katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wake wa kwanza huku pia ikiwachapa Coastal Union mabao 2-0, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kocha Mkuu wa Yanga, Nassredine Nabi, alisema anafahamu mechi hiyo itakuwa ngumu na yenye ushindani kwa sababu Azam FC pia imesajili wachezaji wazuri na wenye uzoefu.

Nabi alisema mabadiliko ya benchi la ufundi ni sababu nyingine itakayowafanya wasifahamu vyema aina ya mfumo ambao wataingia nao wapinzani wao.

"Mchezo hautakuwa rahisi, ni mchezo muhimu kwetu kupata matokeo, tutaingia tofauti, hatutatumia mbinu ambazo tulizitumia katika mechi zetu za ugenini, tutabadilisha mfumo kwa sababu kila mchezo unahitaji mpango kazi tofauti," alisema Nabi.

Naye Mkurungenzi wa Mashindano wa Yanga, Saad Kawemba, alisema kikosi chao kiliendelea kujiimarisha kwa kufanya mazoezi magumu kwa sababu hawakupata muda wa kutosha wakati wa Pre Season.

Aliongeza mechi za kirafiki ambazo wamecheza wakati ligi imesimama zilikuwa na malengo ya kiufundi na si kuangalia matokeo ya mwisho kama inavyotafsiriwa.

Naye Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria, alisema kikosi chao kinaendelea kuimarika na hawana hofu yoyote kuelekea mechi yao dhidi ya Yanga.

"Tunasubiri muda, mazoezi yanayoendelea ni ya kuiweka miili ya wachezaji wetu tayari, lakini kiufundi tulishamaliza kazi," Zaka alisema.

Post a Comment

0 Comments