Ticker

6/recent/ticker-posts

NABI: Nina Uwezo wa Kufundisha Al Ahly au Barcelona

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kiwango chake cha taaluma aliyonayo kinamruhusu sio tu kuinoa Yanga, bali hata klabu kubwa duniani ikiwamo Al Ahly ya Misri au Barcelona ya Hispania.

Nabi ameyasema hayo baada ya kuibuka sintofahamu kuwa hana vigezo vya kukaa benchi la timu hiyo kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini.

Nabi amewashusha presha mashabiki wa timu yake akisema vyeti alivyonavyo sio tu Yanga anaweza kuifundisha hata Barcelona ya Hispania, Al Ahly ya Misri na klabu zozote kubwa duniani zikimhitaji.

Nabi amesema wapo makocha wengi wakubwa wenye leseni kama yake ya Uefa Pro wanazifundisha klabu kubwa Ulaya wakiwemo Carlo Anceloti, Jurgen Klopp, Xavi Hernandez na hata Pep Guardiola.

“Nimeziona hizo taarifa, nimeshangaa, nafikiri ni siasa za soka la hapa Tanzania, wanaosambaza hizi taarifa waambieni kuwa sio Yanga tu, bali hata Barcelona, Al Ahly, Real Madrid, Manchester City zikinihitaji naweza kwenda kuzifundisha kwa leseni niliyonayo,” alisema Nabi aliyewahi kuziona Al Ahly Benghazi ya Libya, Al Hilal na El Marrikh za Sudan na kuongeza;

“Nenda kawaulize Klopp ana leseni gani, nenda kwa Ancelotti (Carlo), Guardiola, Xavi au Jose Mourinho wana leseni ipi, nafikiri kama kuna kitu hakipo sawa, hilo ni swali kwa viongozi wa klabu, kazi yangu ni kuwaandaa wachezaji. Mimi sio kocha mdogo kama wanavyofikiria.”

“Ni bahati nipo hapa Yanga naheshimu hii klabu na mashabiki wake, nimechagua kuwa hapa, ila isiwe nafasi ya watu kunidharau na kuniona kama kocha mdogo hiyo siwezi kunyamaza.”

Nabi amesema anashangaa kuona taarifa hizo huku watu wakisahau kwamba aliiongoza Yanga katika michuano hiyo msimu uliopita, japo alitolewa raundi ya awali na Rivers United ya Nigeria na kama angekuwa na tatizo asingeweza kuiongoza.

“Nilitakiwa kuleta cheti changu ili kuwaonyesha, bahati mbaya vipo nyumbani Ubelgiji, lakini nimewasiliana na watu wa Shirikisho la Ubelgiji wakanitumia nakala hiyo nadhani tayari ilishakwenda CAF (Shirikisho la Soka Afrika),” alisema Nabi akionekara kukerwa na taarifa hizo na kuongeza;

“Kuna mafanikio ambayo tunayapata hapa Yanga ni vyema watu wakaweka heshima kwa makocha, kijana wangu(mwanae) anafuatilia taarifa za hapa katika mitandao akiwa Ubelgiji, ameshangaa sana kuhusu taarifa hizo.”

Nabi anaiandaa Yanga kwa sasa kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar kabla ya kurudiana na Zalan wikiendi ijayo na kama itafuzu itacheza na mshindi wa mechi ya St George ya Ethiopia ama Al Hilal ya Sudan.

Post a Comment

0 Comments