Ticker

6/recent/ticker-posts

"Simba, Yanga zajitoa kusaidia jamii"

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


BAADA ya miamba ya soka nchini Simba na Yanga kutambulisha wadhamini wao wapya, sasa zinapambana kutoa huduma kwenye kijamii.

Timu hizo kongwe za soka nchini, zinaelekea kwenye kilele cha hafla zao za kutambulisha wachezaji wao, jezi na maofisa wao kwa wanachama wao kwa ajili ya msimu mpya.

Yanga wiki iliyopita ilitangaza udhamini wake na kampuni ya kubashiriki ya Sportipesa wenye thamani ya Sh bilioni 12 kwa miaka mitatu kabla Simba juzi haijatangaza udhamini wa kampuni nyingine ya kubashiri ya M-bet wenye thamani ya Sh bilioni 26.1 kwa miaka mitano.

Shughuli hizo zinafanyika kama sehemu ya maandalizi ya matamasha yao ambapo Yanga itakuwa na siku ya Mwananchi Jumamosi hii kabla ya Simba kuwa na Simba day Jumatatu ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Yanga jana ilikuwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani, Dar es Salaam kutembelea wanafunzi wa shule hiyo wakiongozwa na Rais wao Injinia Hersi Said.

Wakiwa shuleni hapo, Yanga walizungumza mawili matatu na wanafunzi na walimu na kutoa vifaa vya shule zikiwemo kalamu, madaftari na vitabu.  

“Yanga ina furaha kubwa sana kuwa sehemu ya kusherehekea siku hii ambayo tumekuja hapa Shule ya Jangwani, sherehe ambazo zinaelekea kuadhimisha Wiki ya Mwananchi ambayo imeanza jana (juzi) Agosti Mosi na tunawaalika wote mshiriki nasi pia siku ya kilele Agosti 6 lakini kusherehekea kwa pamoja na viongozi wa Yanga waliofika hapa,” alisema Hersi.

Katika kilele cha sherehe hizo, Yanga itacheza na Vipers SC ya Uganda. Yanga leo itakuwa na ratiba ya kuchangia damu salama. 

Kwa upande wa Simba, jana ilitembelea kituo cha wazee Nunge kilichopo Kata ya Vijiweni, Kigamboni mkoani Dar es Salaam.

Kituo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1936 kwa ajili ya kuwatunza waathirika wa ugonjwa wa ukoma kina wazee 22, huku 12 wakiwa wanaume na wanawake 10.

Akizungumza katika kituo hicho Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju, aliwapongeza Simba na Mo Foundation kwa moyo wa kujali makundi ya watu waliosahaulika.

“Mlichokifanya sio ibada bali mmeigusa jamii, serikali haina timu lakini inaambatana na vitu vizuri na sisi tunawaombea mema na mmetoa somo kwa timu nyingine.”

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema kuwa Simba inaonesha ukaribu wake kwa jamii na wameamua kuja kwenye kundi hili lililosahaulika sababu wanajua thamani yao.

“Tumesikia changamoto zilizopo ikiwamo uzio na paa, tumemwomba Ofisa Ustawi atuletee taarifa tuone tutawasaidiaje, tuna malengo mengi kuanzia Agosti 8 na 13 pamoja na msimu mzima.”

Post a Comment

0 Comments