Ticker

6/recent/ticker-posts

Kocha Simba Asema wapo tayari kuwakabili Al Hilal

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola Amesema wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya wenyeji, Al Hilal utakaochezwa leo kwenye mji wa Omdurman nchini Sudan.

Itakuwa ni mechi ya pili kwa vigogo hao wa Tanzania katika michuano maalum iliyoandaliwa na Al Hilal baada ya mechi ya kwanza iliyochezwa nchini humo dhidi ya  Asante Kotoko ya Ghana ambapo ilishinda mabao 4-2.

Matola amesema anaamini mechi hiyo itaendelea kuwasaidia wachezaji wake kujiimarisha kuelekea mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazofuata na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo alisema benchi la ufundi linaendelea kufurahia fursa waliyopata ya kushiriki michuano ambayo inawapa nafasi baadhi ya wachezaji waliokosa maandalizi ya pamoja ya Pre Season ambapo waliweka kambi Misri na wengine waliokosa nafasi ya kucheza mechi mbili za awali za Ligi Kuu Tanzania Bara.

"Kocha (Zoran Maki) sasa ameanza kupata picha halisi ya mchezaji fulani yuko vipi na amtumie wapi, hii itatusaidia sana kwenye mechi za Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wachezaji wanazidi kuimarika," alisema Matola.

Simba inacheza michuano hiyo bila ya nyota wake tisa walioko katika kikosi cha timu ya taifa (Taifa Stars), pamoja na Erasto Nyoni ambaye ni mgonjwa na Joash Onyango aliyeachwa hapa nchini.

Al Hilal, ilipata ushindi mnono katika mechi yake ya kwanza ambapo iliwatandika Asante Kotoko mabao 5-0.

Habari njema ni kwamba kiungo mkabaji, Sadio Kanoute, amejiunga na kikosi hicho akitokea kwao Mali alipokwenda kufuatilia suala ya hati za kusafiria.

Endapo Simba itashinda mechi ya leo, basi itakuwa bingwa wa michuano hiyo maalum, lakini ikitoka sare au kufungwa itakuwa imeshika nafasi ya pili nyuma ya wenyeji, Al Hilal.

Januari mwaka jana Simba iliwaalika Al Hilal na TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kushiriki  michuano maalum iliyojulikana kwa jina la Simba Super Cup na wenyeji walitwaa ubingwa.


Post a Comment

0 Comments