Ticker

6/recent/ticker-posts

Msuva Yanga ya msimu ujao itakuwa tishio

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa


NYOTA wa kimataifa wa Tanzania Simon Msuva amekiangalia kikosi cha Yanga na kusema kuwa msimu ujao kitakuwa tishio, ila akawapa neno kuwa ili watishe kimataifa na kuweka rekodi mpya basi lazima wajipange kikamilifu.

Msuva amejiunga hivi karibuni na klabu ya Al Qadisiyah inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, Saudi Arabia baada ya kushinda kesi yake FIFA dhidi ya klabu aliyokuwa akiichezea awali, Wydad Casablanca ya Morocco.

Winga huyo mwenye kasi uwanjani ameitabira Yanga kuendelea kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Bara msimu jao kutokana na usajili mkubwa ilioufanya lakini akawakumbusha ili watishe kwenye michuano ya kimataifa ni lazima wajiandae vizuri, kimazoezi na kisaikolojia.

Alisema wachezaji iliowaongeza kikosini wakiwemo Stephane Aziz Ki (ASEC Mimosas) Lazarous Kambole (Kaizer Chiefs), Bernard Morrison (Simba), Joyce Lomalisa (G.D. Sagrada Esperança) na Gael Bigirimana (Glentoran FC) ni wa kiwango kikubwa na kama wataendana kwa haraka na falsafa ya kocha wao basi timu hiyo itakuwa haishikiki.

“Yanga wako vizuri sana kwani nilichofurahi wale wachezaji wao walioipa mafanikio timu hiyo msimu uliopita, asilimia kubwa wamebaki na pia wameongeza majembe hasa ambayo wakishirikiana na waliopo na kupata muunganiko mzuri kwa haraka basi watakuwa moto sana.

“Kufanya vizuri kwenye ligi msimu ujao sina mashaka nao lakini mashindano ya kimataifa ni tofauti kidogo wanatakiwa kufanya maandalizi makubwa na wachezaji wajitoe mara mbili zaidi uwanjani ili kuipa timu hiyo mafaniko.

“Wasiingie kwenye michuano ya kimataifa kwa kuangalia rekodi yao ya kufanya vizuri msimu uliopita, bali wajipange vizuri sasa kufanya kazi kubwa uwanjani na kisaikolojia pia kwani michuano ya kimataifa ni makubwa na kuna mambo mengi ndani na nje ya uwanja,” alisema Msuva.

Msuva ni mmoja ya wachezaji walioipeleka Yanga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2016 baada ya kuifunga Sagrada Esteranca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1 katika mchezo wa hatua ya mtoano (Play Off) baada ya kutupwa nje kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Winga huyu alifunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 ambao Yanga ilipata katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa huku lingine likifungwa na Matheo Antony wakati kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika Angola Yanga ilichapwa bao 1-0.

Post a Comment

0 Comments