Ticker

6/recent/ticker-posts

Mbinu Za Mayele, Aziz Ki Zamkosha Nabi


MAZOEZI ya Yanga kule Avic, Kigamboni yanaendelea huku dozi ikipunguzwa lakini kuna ushirikiano flani wa mastaa wawili ukamfanya Kocha Nasredinne Nabi kuchekelea na kutamba kuwa wapinzani wao wa ndani na wale wa kimataifa watakuwa na kazi ngumu dhidi ya timu hiyo.

Yanga ambayo leo Jumamosi itaadhimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi shughuli itakayofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kwa kuvaana na Vipers ya Uganda iliyowasili jana Alhamisi, tangu majuzi Yanga ikiwa kambini ilipunguza dozi ya mazoezi kwa kuwa na ratiba ya kujifua kwa mara moja pekee kwa siku.

Hii ni baada ya makocha wa timu hiyo kushtukia kitu kwamba katika mchezo wao wa tatu dhidi ya Namungo juzi licha ya kushinda lakini wachezaji walionekana kuwa wazito.

Hata hivyo, uzito huo ukapunguza dozi ya mabao ambapo timu hiyo ilishinda 2-0 , yakiwekwa kimiani na Fiston Mayele na Heritier Makambo na kuwafanya mabingwa hao kutimiza jumla ya mabao 16-1 katika mechi zao tatu walizocheza hadi sasa wakiwa kambini.

Lakini jana Kocha Nabi akaliambia Mwanaspoti kuwa ingawa bado hajavutiwa na ubora wa kikosi chake lakini kuna maendeleo makubwa hasa katika eneo la ushambuliaji kwa nyota wake, Stephane Aziz KI na Mayele waliomkuna zaidi.

Nabi alisema amekoshwa na kuvutiwa zaidi na ushirikiano wa wachezaji hao na kuona wakianza kushiriki mechi za mashindano wapinzani wa timu hiyo watapata tabu sana.

“Wanavutia ukiona wanavyocheza wanashirikiana vizuri uwanjani, hiki ni moja ya kitu nilichokuwa nakitaka, ingawa bado wanatakiwa kuimarika zaidi na nitaendelea kuwapa mbinu zaidi ili eneo la mbele liwe na makali kuliko msimu uliopita,” alisema Nabi ambaye inaelezwa amekubaliana na Yanga kusalia kikosi kwa kupewa mkataba mpya wa miaka miwili.

“Wapo wengine wanacheza kwa maelewano zaidi na kuleta faraja ukiangalia eneo la kiungo pia na hata safu ya ulinzi, lakini hii kombinesheni ya Aziz KI na Mayele imekuna zaidi na ninaona Yanga tukija na moto zaidi,” alisema Nabi aliyeiongoza Yanga katika mechi 37 za Ligi Kuu kwa misimu miwili iliyopita bila kupoteza na kusaliwa na michezo miwili tu kuipiku rekodi ya Azam iliyoweka kwa kucheza mapambano 38 mfululizo kuanzia Feb 2013 hadi Okt 25, 2014.

Nabi alisema anaamini Yanga itazidi kuimarika watakapoendelea kunoa makali baada ya mechi ya tamasha kwa kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambao msimu uliopita waliifumua bao 1-0 kupitia Mayele.

Mayele katika mechi tatu za kirafiki za maandalizi ya msimu huu, aliendeleza moto wa mabao yake akifunga matano, huku Aziz Ki akifunga bao moja na kutengeneza asisti tatu likiwemo bao la Mayele alilowafunga Namungo juzi wakitangulia kugongeana vizuri.

Aidha Nabi alisema bado anasubiri kuimarika kwa winga Bernard Morrison ambaye alichelewa kuanza mazoezi na wenzake.
Manzoki ndani ya nyumba

Vipers imeshatua nchini jioni ya jana kwa ajili ya mechi ya kesho ya kilele cha Wiki ya Mwananchi ikiwa jeshi kamili akiwamo straika, Cesar Manzoki aliyekwama kujiunga na Simba msimu huu kutokana na klabu hiyo ya Uganda kutaka mkwanja mnene kumuachia kwani bado ana mkataba.

Vipers imekuja na wachezaji 21 na iliwasili saa 10:30 ikiwa pamoja na Manzoki ambaye inaelezwa atajiunga na Simba katika dirisha dogo wakati akiwa mchezaji huyo.

Wengine waliopo kwenye msafara wa mabingwa hao wa Uganda ni Makipa Fabien Mutombora, Alfred Mudekereza na Dennis Kiggundu, huku mabeki wakiwa ni Halid Lwaliwa, Livingstone Mulondo, Dissan Galiwango, Hilary Mukundane, Isa Mubiru na Ashraf Mandela.


Viungo ni Bobosi

Byaruhanga, Bright Anukani, Marvin Joseph, Siraje Sentamu, Olivier Osomba, Ibrahim Orit na Abdulkarim Watambala, wakati safu ya ushambuliaji inaundwa na Manzoki, Yunus Sentamu, Milton Karisa, Najib Yiga na Abubakar Lawal.

Huu utakuwa msimu wa nne kwa Yanga kufanya tamasha la Wiki ya Mwananchi na msimu uliopita ilivaana na Zanaco kwenye mechi kali na kulala mabao 2-1.

Post a Comment

0 Comments