Ticker

6/recent/ticker-posts

Yanga yaongeza dozi kuelekea mchezo dhidi ya Azam FC

Kwa maombi ya kazi, Bofya hapa

Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameongeza dozi kwa kutumia dakika 90, katika programu yake kuwapa wachezaji wake mazoezi mazito ya gym na ufukweni kwa ajili ya kuimarisha stamina.

Kikosi hicho cha Yanga kilionekana kikifanya mazoezi hayo magumu juzi na jana asubuhi katika gym ya Gymkhana jijini Dar es Salaam na jioni wakiendelea kujijenga kwenye viwanja vya Avic Town ambapo wameweka kambi.

Wakati akihojiwa Kocha Nabi, alisema amepanga kuwapeleka nyota wake katika ufukwe wa Coco ili kuendelea kuwanoa kwa sababu anahitaji wawe fiti na tayari kuwakabili Azam FC.

Nabi, alisema anataka kuona wachezaji wake wana pumzi ya kutosha na ndio programu maalumu aliyowaandalia nyota wake katika kipindi hiki cha mapumziko.

"Nahitaji kuwa na kikosi bora na chenye uwezo mkubwa wa kupambana katika dakika zote za mchezo, mazoezi ya viungo  ni muhimu kwa sababu yanajenga utimamu wa mwili na kuwaweka imara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mechi,".

“Napambana kujenga kikosi bora kwa sababu nahitaji kuwa na timu imara katika msimu huu ambao tumedhamiria kupambana kupata matokeo mazuri katika michezo yote tutakayocheza,” alisema Nabi. 

Kocha huyo aliongeza hataki kuona nyota wake 'wanakata' pumzi katikati ya mchezo na endapo hilo litatokea itawaweka kwenye wakati mgumu.

"Ninataka kikosi kiwe na uwezo wa kucheza katika kiwango cha juu, ndio maana tunapambana kuhakikisha wanakuwa imara na vile vile wana pumzi ya kutosha wakati wote, tunahitaji kuwa bora kuliko tulivyokuwa msimu uliopita," Nabi alisema.

Yanga inajiandaa kuvaana na Azam FC katika mechi ya raundi ya tatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Septemba 6, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1.00 usiku.

Baada ya mchezo huo, Yanga itaendelea na maandalizi ya kuwavaa Zalan FC, kutoka Sudan Kusini katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Septemba 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na marudiano yakifanyika katika uwanja huo huo.

Simba inayonolewa na Mserbia Zoran Maki, ndio vinara wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 wakifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga, kila moja ikiwa na pointi sita mkononi.


Post a Comment

0 Comments